Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dodoma

Serikali imemwagiza Kamishna wa Elimu,Mkurugenzi wa Udhibiti ubora wa Elimu na Mwanasheria wa Wizara ya Elimu kufanya uchunguzi wa tukio la vitendo vya watoto kufundishwa kulawitiana katika baadhi ya shule nchini.

Hayo yamesemwa na leo Januari 17, 2023 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na kuripotiwa kwa tukio hilo kwenye vyombo vya habari.

Mkenda amesema kuwa Serikali haitafumbia macho vitendo visivyo na maadili vinavyofanywa na katika baadhi ya shule kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Waziri Mkenda amesema kuwa timu iliyokwenda italeta taarifa kamili na wapo tayari kuchukua hatua stahiki kudhibiti mambo hayo.

“Tumeshitushwa sana na taarifa hizo,tumeamua kumpeleka Kamishna wa Elimu mwenyewe siyo mwakilishi wake,Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Elimu mwenyewe siyo mwakilishi wake pamoja na mwanasheria wa wizara waende haraka sasa hivi wanapitia kwenye hizo shule zilizotajwa kujaribu kupata ukweli wote ”amesema Prof. Mkenda.

Mkenda amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, kusaidiana na timu hiyo ili katika maeneo ambayo yananahusisha masuala ya jinai Polisi wachukue hatua mara moja.

Aidha Waziri Mkenda ameongeza kuwa Wizara imekusudia kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa namba maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa ya vitendo hivyo katika shule za umma au binafsi nchini.

“Kesho Katibu Mkuu wa Wizara atatoa namba ambayo mtu yeyote ambaye akijua kuna kitu kama hicho katika shule yeyote iwe ya umma au binafsi au vyuo vyovyote hapa nchini apiga simu na kutoa taarifa,” amesema .

Hata hivyo ameongeza kuwa watafuatilia kwa nchi nzima mambo haya kwa sababu yanaweza kuchafua taswira ya elimu pamoja na kuharibu vijana na hata wazazi kukosa imani.

By Jamhuri