Serikali:Uchunguzi ajali ya ndege kukamilika ndani ya mwaka mmoja

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Serikali imetoa maelekezo kwa wataalamu wa ndani ya nchi kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha ajali ya ndege iliyotokea Bukoba.

Taarifa hiyo imetolewa leo Novemba 14,2022 jijini Dodoma na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ambapo ameeleza masuala mbalimbali yaliyojadiliwa wakati wa kikao hicho cha dharura cha Baraza la Mawaziri.

Msigwa ameeleza kuwa kikao hicho kimeelekeza vitengo vyote vinavyohusika na majanga nchini viimarishwe ili viweze kusaidia wakati wa majanga.

Wakati wa kikao hicho cha dharura cha Baraza la Mawaziri, Serikali imewaomba wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea, ili kubaini chanzo cha ajali hiyo ya ndege iliyotokea Bukoba mkoani Kagera na kusababisha vifo vya watu 19, ambapo 24 waliokolewa.

Kikao hicho cha dharura cha Baraza la Mawaziri pia kimepokea taarifa ya awali kuhusu ajali hiyo ya ndege ya Precision na hatua zilizochukuliwa baada ya kutokea kwa ajali hiyo.

“Baraza la Mawaziri limetoa maelekezo haya kwa kuzingtia kwamba nchi yetu imetiliana saini katika mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo inasimamia usafiri wa anga na hatua zinazopaswa kuchukuliwa mara baada ya ajali ya anga kutokea.”

“Kwa hivyo ni mwendelezo wa kutekeleza makubaliano hayo ndo maana Baraza la Mawaziri limeelekeza wataalamu wetu wa ndani washirikiane na wataalamu kutoka nje ya nchi katika kufanya uchunguzi na baadaye watatoa taarifa juu ya chanzo cha ajali na hatua zinazopaswa kuchukuliwa,’ amesema.

Msigwa ameeleza kuwa Baraza la Mawaziri limeelekeza vitengo vyote vinavyohusika kukabiliana na majanga kuimarishwa kwa mambo mbalimbali ambayo itaiwezesha nchi kukabiliana na majanga pale yanapotokea.

“Baraza la mawaziri pia limeelekeza vitengo vitengo vyote vinavyohusika kukabiliana na majanga viimarishwe, kwa mambo mbalimbali ambayo yatatuweshe sisi kama nchi kuongeza uwezo zaidi ya tulio nao katika kukabiliana na majanga pale yanapotokea” amesema.

Akitolea ufafanuzi wa namna mchakato wa uchunguzi wa ajali hiyo utakavyofanyika mpaka kuwasilisha majibu Msigwa ametaja hatua tatu zitakazofutwa ambapo litachukua takribani miezi 12 kukamilika

“Hatua ya kwanza ni timu ya uchunguzi wa ndege ambayo inafanya uchunguzi wake na inatoa maelezo ya awali yaani ‘Accident Bulletin’ ndani ya siku 14 lakini hii inafuatiwa na ripoti ya awali yaani ‘Preliminary report’ ambayo inatolewa ndani ya siku 30 na hatimaye tutamaliza na ripoti kamili yaani ‘Final report’ ambayo ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea.” amesema.

Vilevile amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu katika kipindi chote hiki cha uchunguzi mpaka pale utakapokamilia pia amewashukuru wote walihusiaka kujitoa kuokoa lakini pia kukabiliana na madhara ya ajali ya ndege ya Precision.

Ikiwa ni takribani siku nane zimetimia tangu ndege Shirika la Precision Air ipate ajali kwa kudondoka ndani ya ziwa Victoria ikiwa ni takribani mita chache kutoa uwanja wa ndege wa Bukoba.

Ndege hiyo aina ya ATR 42-500 yenye namba za usajiri PW 494 ilikuwa ikifanya safari zake kutoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza kupitia Bukoba ambapo ndipo ilipata ajali.