Watu 13 wanahofiwa kupoteza maisha na wengine 14 wakinusurika kifo baada ya kuzama ziwa Victoria eneo la Mchigondo kata ya Igundu Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Igundu, Sumila Nyamkinda Kafumu amesema tukio hilo limetokea Julai 30, 2023, majira ya saa 12:00 jioni wakati waumini wa Kanisa Takatifu la Mungu la Kiroho (KTMK) wakiwa wanarejea nyumbani baada ya shughuli za kanisa kukamilika katika kijiji cha Mchigondo.

Kafumu amesema inasadikiwa walikuwa jumla ya watu 28 ambao walipanda mitumbwi miwili tofauti lakini wakiwa safarini mtumbwi wa mbele ulipata ajali na kuanza kuzama ndipo mtumbwi uliokuwa nyuma ulifika kutoa msaada lakini ulielemewa baada ya watu wengi waliokuwa wakitapatapa kuuvuta kwa nyuma wakipambana kujiokoa jambo lililopelekea mtumbwi huo pia kuzama.

Baadhi ya viongozi wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano walifika katika eneo hilo na kuandelea na juhudi za utafutaji ambapo hadi kufikia mchana jana zoezi la utafutaji limesitishwa kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya kutokana na upepo huku wakiweka mipango ya kuendelea na zoezi hilo hapo baadaye kwa ushirikiano wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara na wanatarajia kupata msaada zaidi kwa kikosi cha wanamaji kutoka Mwanza ili kuongeza nguvu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amesema kuwa zoezi la utafutaji wa miili ya watu linaendeleo huvyo amewaomba wananchi kuwa watulivu.

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Augustino Magere amesema tangu walipofika eneo la tukio jitihada za kuwatafuta watu 13 wanaohofiwa kufa maji zimefanyika ambapo hadi saa saba mchana jana hawakufanikiwa kumpata mtu huku changamoto kubwa katika eneo la uokozi ni kuwa na matope mengi.

Wananchi wakifuatilia zoezi la utafutaji watu 13 ambao wanahofiwa kuzama majini.
Mitumbwi inayotajwa kutumiwa na watu hao wakati wa safari ikiwa imetolewa na kusogezwa ufukweni katika kijiji cha Mchigondo.

By Jamhuri