Pancrace ShwekelelaHoma ya uchaguzi imeikumba wilaya mpya ya Kyerwa, ambapo sasa Pancrace Shwekelela anasema “wakati ukifika nitatangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Kyerwa baada ya kushawishiwa na watu, vikundi na marafiki zangu.”
Jimbo la Kyerwa kwa sasa linashikiliwa na Eustace Katagira (CCM). Amekuwa mbunge wa Kyerwa kwa miaka 10. Katagira alilikomboa Jimbo hili kutoka kwa mbunge wa Upinzani, Benedicto Mutungilehi (TLP) mwaka 2005.
Shwekelela ameliambia JAMHURI kuwa ameombwa na watu mbalimbali kugombea ubunge kutokana na sifa ya utendaji wake, ukaribu na wananchi na elimu – ambapo ana shahada ya uchumi na mazingira.
Amesema wakati wa kugombea ukifika, kaulimbiu yake itakuwa ni; MAENDELEO NI KUPANGA NA KUTEKELEZA PAMOJA. Ametaja mambo ya msingi atakayoyapa kipaumbele kuwa ni kuinua uchumi wa Wanakyerwa na kupunguza umasikini.
Shwekelela anasema uchumi wa Kyerwa unategemea kwa kiasi kikubwa zao la kahawa ambako zao hilo linazalishwa kwa wingi kuliko Wilaya zote za Mkoa Kagera.


Anafafanua kuwa kahawa inayolimwa Kyerwa inanunuliwa na kampuni kubwa tatu ambazo ni Oram, Karagwe Eastate na Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Karagwe (KDCU) Ltd vikifuatiwa kwa mbali na KADERES na kwa bei ndogo.
Anasema atapigania soko huria la kahawa kwa nia ya kupandisha bei na kumnufaisha mkulima. Akichaguliwa atahakikisha mkulima anauza kahawa yake popote anakotaka bila kuwekewa vizuizi na halmashauri ibaki kutoza ushuru kahawa kama mazao mengine.
Upande wa kina mama na vijana, Shwekelela anasema atahakikisha wanapata mikopo kwa wakati mwafaka ambayo inatengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kila mwaka kiasi cha zaidi ya Sh 30 milioni.


Zipo taarifa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, haijatoa mikopo hiyo kutokana na kwamba hakuna makundi ya kina mama na vijana waliojipanga kuipokea kwani ni muda mfupi wilaya hiyo tangu ianzishwe hivyo yeye atalisimamia hilo.
Kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi anasema kwa upande wa elimu, Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa yote haina chuo chochote cha ufundi na kwa mawazo yake angependa walau kila tarafa iwe na chuo cha ufundi vijana waliomaliza elimu ya msingi na sekondari wasome na wapate nafasi za ajira binafsi.
Anaongeza kuwa vijana walio wengi hawapati fursa ya kujiajiri kwani asilimia kubwa ya wakazi wa Kyerwa kutegemea kilimo hivyo baadhi ya vijana wanategemea uendeshaji wa pikipiki maarufu bodaboda kujipatia kipato.


Shwekelela anayekusudia kutangaza nia anasema endapo Wanakyerwa watamkubalia kuwa mwakilishi wao, upande wa afya atahakikisha dawa zinapatikana kwenye zahanati na vituo vya afya na kwamba atashawishi wananchi wajiunge na mfuko wa Bima ya Afya.
Anasema atasimamia matumizi bora ya ardhi na kuweka mazingira safi ya wakulima na wafugaji kuepusha migogoro kati yao na atasimamia upimaji wa viwanja hasa maeneo ya miji kwa kila tarafa.
Kuhusu urasimishaji wa ardhi za vijiji chini ya sheria Na 5 ya Mwaka 1999 inayosema wananchi watapata hati za kimila zitakazotumika kupata mikopo kutoka katika benki mbali mbali na kwa riba nafuu, anasema hilo atalisimamia.
Shwekelela anasema Wilaya ya Kyerwa inayo madini ya kutengeneza mabati (TIN) ambayo wananchi hawafaidiki nayo kiasi cha kutosha na mfumo wa ajira hauwalengi Wanakyerwa moja moja hivyo atahakikisha unawalenga Wanakyerwa.


Kwake yeye, anaona Kyerwa ina tatizo kubwa la upatikanaji na usambazaji wa maji ambalo suluhu yake ni kufanya utafiti wa vyanzo vipya vya maji vilivyoko na kufufua miundombinu ya maji iliyoharibika. Kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza adha ya ununuzi wa maji na kupunguza tatizo la maji ndani ya wilaya hii.
Mtarajiwa huyo atakayetatangaza nia wakati ukifika, katika suala la miundombinu anasema atajikita zaidi kwenye barabara za vijiji na kata kuwezesha mawasiliano na usafirishaji wa mazao ya wakulima kutoka walipo hadi kwenye masoko wanakotaka kuuza mazao yao.
Shwekelela  anasema upande wa watumishi mbalimbali ambako yeye amekuwa mtumishi serikalini kwa zaidi ya miaka 20 anafahamu matatizo ya watumishi yanayohitaji  ufumbuzi wa haraka ikiwa ni pamoja na mishahara, upandishwaji wa vyeo na madaraja.


Anasema hayo anayowaza atayasimamia kwa karibu hasa kwa kuwafikia wahusika ambao ni waajiri mbalimbali kuhakikisha wafanyakazi wananufaika na jasho lao.
Akielekeza upande wa michezo, Shwekelela anasema atahakikisha michezo iliyolala inafufuliwa kama mpira wa pete, wavu, kikapu, mpira wa meza na mpira wa miguu na michezo mingineyo ambayo lengo ni kuinua vipaji kila mwaka badala ya mpira kuchezwa kiligi baada ya miaka mitano.
Kuhusu vyanzo vya mapato ya kuendesha michezo, anasema wataanza kwa kutenga bajeti kila mwaka katika Halmashauri ambapo akiwa mbunge atalisimamia hilo na kutafuta wafadhili mbalimbali na wapenda michezo.

 
4024 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!