Wagombea vijanaTaifa linatarajia mabadiliko makubwa katika uchaguzi wa mwaka huu! Gazeti la Mwananchi Toleo No. 5419 la Jumatano Mei 27, 2015 uk. 33 limeelezea hoja zinazojitokeza kuhusu umri wa wagombea.  “HOJA ZA UJANA, UZEE katika vuta nikuvute uongozi wa Tanzania” habari kamili iliandikwa katika uk.  wa 36.
Hapa ingefaa tuone busara za uongozi uliopita ulitathmini namna gani uzee na ujana wa wagombea uongozi. Namnukuu Rais wa Awamu ya III na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mwaka 1995 – 2005, Benjamin William Mkapa alisema hivi:
“…umri unapaswa kuzingatiwa kutokana na ukweli kwamba wapigakura wengi ni vijana. Mkapa hakuibuka tu na hoja ya umri, bali alijawa na hofu na namna Freeman Mbowe (CHADEMA) aliyekuwa akishabikiwa na makundi ya vijana kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu (2005). Pia alitishwa na kundi la wanamtandao kwamba ikiwa mgombea kijana na mwenye ufuasi mkubwa ataachwa, upinzani utaingia Ikulu kirahisi…” (Tazama Mwananchi toleo No. 5419 la Jumatano, Mei 27, 2015 uk. 36).


Mwaka 1958 – 1960 vijana wa Tanganyika walijiamini na walikuwa tayari kupokea dhamana ya utawala wa nchi hii kutoka kwa wakoloni.
Vijana wetu wa leo wanajiandaaje kuingia katika uongozi wa nchi hii? Ninachokiona siku hizi ni vyama vya siasa kuandaa vijana wao kwa ulinzi wa kura siku ya uchaguzi.
Kila Chama kina kikosi cha ulinzi eti kuwalinda viongozi na kulinda kura zisiibwe. Hili linanishangaza. Vipo vikundi vinavyoitwa Green Guards, Blue Guards na Red Brigade.
Wanaandaliwa kiulinzi, lakini siyo kupokea madaraka ya uongozi pindi wazee katika vyama hivi wataamua kung’atuka. Je, yapo malezi au makuzi kwa vijana kuandaliwa kupokea madaraka ya utawala ndani ya Chama na katika Serikali?


Je, sasa wakati wa uchaguzi ujao Oktoba mwaka huu, hii hali itakuwa tofauti na ile ya 2005? Hakuna wanasiasa wenye ufuasi mkubwa na mtandao uliokamilika kama ule wa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005? Hali namna hii wangoni tunaita “Ndindani” yaani hali ya kutokueleweka nini kifanyike.
Hapo vyama vya siasa vyote vipo katika hali ya “sintofahamu” kinachoendelea au nini kitatokea. Hakuna anayeweza kujua wala kutabiri “RAIS MTARAJIWA” wa Tanzania atakuwa nani.  Tuna mitazamo tofauti. Kuna viongozi wameapa hawang’atuki mpaka wameingia Ikulu siku moja.
Kugombea nafasi ya uongozi zaidi ya mara moja ni jambo la kawaida, maana kwa viongozi wa namna hii, Chama siyo taasisi bali ni mali ya mtu binafsi. Lakini kuna mazoea katika nchi hii kuwa kila kitu kiende kwa ile sera “HURIA”.


Hii sera huria katika biashara imeonekana kuliletea taifa hili matatizo makubwa katika uchumi. Bidhaa feki zinaingizwa. Kila mtu yuko huru kuuza chochote na popote katika Tanzania. Matokeo yake hata wageni kutoka nje wanauza ubuyu, maua, midoli pale Kariakoo, huo ni ubaya wa biashara huria.
Utandawazi  na biashara huria vimeingizwa mpaka katika elimu na tiba hapa nchini. Kila mtu ama taasisi inaweza kufungua shule au hospitali binafsi na kuuza huduma husika kwa wenye pesa tu.
Lakini tukiwa na siasa huria, naona pana hatari kubwa hapa nchini. Vitachipuka vyama vya siasa kama unavyochipuka uyoga msituni. Utitiri wa Wanasiasa watajitokeza kugombea nafasi za uongozi.


Tumeshasikia Kigoma au Loliondo kumetokea wageni toka nchi jirani wamegombea uongozi katika Serikali za Mitaa na kufanikiwa kupata uongozi huo. Je, ikitokea mgeni kugombea ubunge au Urais nini kitamzuia? Hizo ndizo bahati mbaya za sera ya siasa huria.
Na kama vijana wangeandaliwa vizuri kiitikadi, uzalendo na maadili mema sina shaka vijana wa kuongoza vyama wangeweza kuongoza taifa letu kwa mafanikio makubwa.
Kwa kukosekana kwa maandalizi namna hii kwa vijana vyama vinajikuta vinashindwa kuwa na mrithi wa uongozi wa wazi wazi ndani ya vyama vyote.


Ni tatizo la ubinafsi hili. Matokeo ya hali namna hii ndiyo hayo tunayaona sana, viongozi kadhaa toka chama kimoja wanajitokeza kutaka urais. Hii siyo siasa huria bali ni siasa holela.
Ninajua baadhi ya wazee hawatapenda haya ninayoyaandika. Lakini tangu zamani za kale, kuna wanafalsafa wa kirumi walisema hivi, kwa kilatini, “…tempora mutantur, nos et mutamur in illis” yaani nyakati zinabadilika nasi twende na mabadiliko hayo ya nyakati – yaani tubadilike.
Hapo wazee si inatupasa twende na wakati? Huu ni wakati wa mabadiliko ya utawala – tukubali sote mabadiliko hayo yanawezekana kama kuna uongozi shupavu na makini.


Hapo basi hali ile ya hoja za ujana, uzee katika vuta nikuvute ya uongozi wa Tanzania isingalitokea asilani. Urithi wa uongozi katika chama ungejulikana wazi wazi yupi atarithi kiti kile. Kwa utaratibu namna hii wagombea uongozi – Urais watajiwa kamwe wasingekuwa wengi kama ilivyo leo hii.
Vijana (wako very flexible), wana unyumbufu wa maisha na wa miili yao, hivyo wanaweza kuongoza.  Matumaini yetu wazee ni kumwomba Mwenyezi Mungu uchaguzi ujao ufanyike kwa utulivu na amani.
Vyama viteue viongozi wanaokubalika miongoni mwa watu. Wateuliwa wawe na maadili mema, wamuogope Mungu na wawajibike kwa sisi wananchi tuliowachagua.
Umri wa mgombea kisiwe kigezo pekee. Lakini vyama visiteue wazee ving’ang’anizi wa madaraka hawatamudu harakati za utandawazi katika dunia ya leo.


Aidha vyama visiteue wala rushwa maana Mwalimu alikemea rushwa kuwa ni ufa Na. 4. Alielezea kinaganaga katika yale mazungumzo yake na waandishi wa habari pale Kilimanjaro Hoteli Machi 13, 1995.
Labda ninukuu maneno yake yale hapa, alitamka hivi, “…Sasa Tanzania inanuka kwa rushwa. Tunataka kiongozi anayejua hivyo na ambaye atasema, “rushwa kwangu ni mwiko” mwaminifu kabisa, hawezi  kugusa rushwa na wanamjua hivyo watoa rushwa…”
Lakini sasa katika uchaguzi nasikia mtu anakuja na pesa. Uchaguzi mwaka huu utakuwa uchaguzi wa pesa. Zamani katika CCM na katika TANU tunapochagua mgombea wetu, kama ana mali, tunamwambia, “hii mali umepata wapi?”


Mali ilikuwa kigezo cha kukupotezea sifa ya kuwa mgombea. Mwaka huu 2015 mali itakuwa ndiyo kigezo namba wani. Wanazipata wapi?  Wamepata wapi?… (Nyerere: Nyufa uk. 20 – 21, Kilimanjaro Hoteli tarehe 13 Machi, 1995).
Sasa Tanzania inahitaji kiongozi shupavu, mwenye ujasiri na moyo wa kuthubutu kutenda. Awe basi mruturutu wa kuzuia rushwa na atujengee uchumi kwa kuondoa umaskini wa wanyonge wa nchi hii.
Jambo kubwa na zito katika uchaguzi ujao ni idadi ya wapiga kura katika daftari lililoboreshwa. Kusijetokea kura za maruhani katika nchi hii kuwapa ushindi wasiostahili.


Hakuna haja ya ulinzi wa green guards wala blue guards wala Red Brigade. Polisi watafanya kazi gani? Wasiwasi wa viongozi wa vyama unatokana na ile methali ya kiingereza isemayo “set a thief to catch a thief” yaani mtumie mwizi kumnasa mwizi mwenzake! Ndiyo kusema wasioaminiana, basi wote wana mwelekeo huo huo wa wizi. Hiyo ndiyo sababu kubwa ya Vyama vya Siasa kutokuaminiana katika mambo haya ya Uchaguzi.
Tumefikia hali ya namna hiyo watanzania kutokuamiana kweli? Hapo naweza kusema hali inatisha katika nchi yetu. Bila kuaminiana kuna jenga woga na tuhuma zisizokuwa na msingi.
Hapo ndipo yanajengeka mazingira ya mvunjiko wa amani nchini. Kiongozi ajaye aweze kuamua kwa mkato ili kuondoa hali ya sintofahamu hapa nchini.


Bado nina tumaini kuwa Uchaguzi wetu mwaka huu utakwenda vizuri tu. Juzi juzi tarehe 07/05/2015 Uingereza walipiga kura. Tumeona matokeo. Lakini siyo Waingereza wote wameyapokea. Kutokana na hali hiyo tumeona pale London tarehe 09/05 watu wameandamana kupinga matokeo yale eti hawamtaki Waziri wao Mkuu aliyeshinda kwa kishindo – Chama chake kimeshinda.
Kama huko kwa wakubwa bado watu wanalalamikia matokeo, sembuse sisi? Kule wale wenzetu wanauzoefu mkubwa sana wa Uhuru wa Uchaguzi katika demokrasia yao.
Sisi huu utakuwa ndio Uchaguzi wetu wa nane (8) tu kwa vyama vingi (1958, 1960, 1962, 1995, 2000, 2005 na 2010) kadiri ya kumbukumbu zangu. Chaguzi zile nyingine 1965, 1970, 1975, 1980, 1985 na 1990 zilikuwa za Chama kimoja tu. Je, kweli tuna uzoefu wa kutosha katika chaguzi za kidemokrasia? Kwa nini zisitokee dosari nasi tukazivumilia?


Tunataka demokrasia yenye ufanisi wa hali ya juu (perfection) jambo ambalo hata huko tulikoiga hizo chaguzi za kidemokrasia hakuna! Uingereza wamelalamikia matokeo. Marekani wakati wa Bush matokeo ya Florida yalilalamikiwa. Sasa sisi ulimwengu wa tatu tusitumaini miujiuza.
Tuwe watulivu na tujifunze kurekebisha dosari zitokeazo katika chaguzi. Uingereza ni Polisi tu waliosimamia amani na utulivu katika huo Uchaguzi wao mkuu.
Tujifunze kupokea matokeo ya kura kwa amani wala tusiendeleze yale mazoea yetu ya kutokupokea matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi. Kupevuka kisiasa ni pamoja na kukubali matokeo ya kura.
Tumeona Nigeria, Jonathan alikubali matokeo ya kura mapema na akampongeza Jenerali Buhare. Huo ni ukomavu wa demokrasia nchini Afrika. Kumekuwa na utulivu. Kutokukubali matokeo ni dalili kubwa ya kutokupevuka kisiasa (political immaturity). Watanzania tuoneshe sasa tumekomaa, tunayo demokrasia ya kweli.  Tujiandae kuonesha Afrika tulivyokomaa kisiasa.


Katika ulimwengu wa leo nchi za Afrika ziwe tayari kupokea mabadiliko katika utawala. Kutokuwa tayari kwa mabadiliko ndiyo chanzo cha mifarakano na mapambano katika nchi.
Kutokubali kuwa wapo wengine wenye uwezo wa kuendesha gurudumu lile la maendeleo katika nchi ni ugonjwa wa viongozi kadhaa katika nchi za Afrika. Je, nasi watanzania tunakubali kuwemo miongoni mwa wagonjwa namna hiyo?
Mungu atuepushe na balaa la ghasia maana tutakuwa wageni wa nani? Tumezowea kupokea wakimbizi na wapigania Uhuru. Basi haiingii akilini mwa mtanzania kufikiria kuwa kuna siku eti naye atakuwa mkimbizi.


Kuepukana na hali hiyo tudumishe Amani na utulivu. Nchi yetu ni kama kioo cha demokrasia barani Afrika. Tujiepushe na kishawishi cha “tusiposhinda sisi safari hii basi hatutakubali matokeo ya kura za mwenye masanduku”. Je, kwa matamko namna hii kutakuwa na Amani Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu? Hapana! “Basi sote tuseme “Tanzania bila mtafaruku au bila mapambano ya umwagaji damu inawezekana”. Na ukitamka Tanzania maana yake unatamka Amani na Utulivu.
“SAMBANO KUCHELE” yaani sasa kumekucha basi hakuna sababu ya kuwa na woga au hofu. Kukiwa kweupe kila kitu kitaonekana wazi. Tuchangamkie uchaguzi ujao; Mungu ibariki Afrika.

>> ITAENDELEA>>

Mwandishi wa Makala hii, Francis Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.

 
2138 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!