Katika hali isiyo ya kawaida, Klabu ya Soka ya Simba imetamba na kuapa kwamba haitathubutu kuwauza hata kwa dau kubwa kiasi gani, wachezaji wake, Amissi Tambwe na Jonas Mkude, kwa klabu yoyote ya hapa Tanzania.

Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga, hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari akisisitiza kuwa klabu za hapa nchini hazina hadhi ya kuwanunua wachezaji hao.

“Kama kuna timu inawahitaji wajue hawapati kitu na hatuna muda wa kuzungumza nao kwani hawa ni wachezaji wetu na tunahitaji mchango wao katika timu,” alisema Kamwaga na kuongeza:

“Tunaweza kuwauza pengine nje ya nchi, tena kwa dau kubwa, kwa maana hatuwezi kukataa ofa nzuri kutoka nje ya nchi bila sababu, huko tunaweza kuwauza, lakini siyo kwa klabu za humu ndani.”

Kamwaga alisema Klabu ya Simba haiwezi kuwauza nyota hao kwa klabu wanazoshindana nazo kwa sababu wanajua na wameona madhara yake, hivyo kama kuna timu ilidhamiria kuwasajili iandike maumivu.

“Kila mchezaji ana bei yake hapo, Tambwe na Mkude tunaweza kuwauza nje ya nchi tena kwa dau kubwa, lakini siyo Tanzania, tena kwa timu tunazoshindana nazo.”

Kauli hiyo ya Simba imekuja baada ya Azam FC kuwasajili Didier Kavumbagu na Frank Domayo waliokuwa wachezaji huru wa Timu ya Soka ya Yanga.

Klabu ya Yanga pia ilihusishwa na mipango ya kuwasajili Tambwe na Mkude ili kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Binafsi ninaitafsiri kauli hiyo ya Klabu ya Simba kwamba ni lugha ya dharau inayozibeza klabu za soka za hapa Tanzania, hali ambayo inajenga taswira ya kudhoofisha maendeleo ya mpira wa miguu hapa nchini.

Kauli ya Klabu ya Simba kwamba haiko tayari kuwauza Tambwe na Mkude kwa klabu ya hapa nchini inadhihirisha jinsi Wekundu hao wa Msimbazi jijini Dar es Salaam wasivyothamini soka la Tanzania.

Dhana hiyo iliyojengwa na Klabu ya Simba inaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa kukwaza hamasa ya maendeleo ya soka hapa nchini katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa wa michezo duniani.

Inavyoonekana Klabu ya Simba haijui hata usemi wa Waingereza kwamba ‘charity begins at home’, ambao kwa tafsiri rahisi unamaanisha kwamba upendo huanzia nyumbani. Klabu ya Simba imekosa upendo wa nyumbani kwao, Tanzania!

Lakini kwa upande mwingine, Klabu ya Simba inapobeza na kuamini kuwa klabu za soka za hapa Tanzania hazistahili kununua wachezaji wazuri, tafsiri yake ni kwamba hata yenyewe haina hadhi ya kumiliki na kuwa na wachezaji wazuri.

Tunajua kwamba Tambwe na Mkude wamebakiza mkataba wa mwaka, na inaaminika kwamba wachezaji hao ndiyo wanaoibeba Simba katika mashindano mbalimbali.

Lakini furaha ya Klabu ya Simba ya kumiliki nyota hao haikupaswa kuvuka mipaka kiasi cha kuthamini klabu za nje na kuamini kimakosa kwamba hakuna klabu ya soka ya hapa Tanzania yenye hadhi ya kuwanunua wachezaji hao.

Tambo, imani na dharau za aina hiyo haziwezi kuhamasisha na kuleta mapinduzi ya kweli katika klabu za soka Tanzania, badala yake zitachangia kukwaza kama si kudidimiza maendeleo ya tasnia hiyo hapa Tanzania. Ama kweli mvunja nchi ni mwananchi!

0689 916 970

1489 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!