Na Mwandishi wetu, Jamhuri Media, Dar es Salaam.

Ikiwa ni muendelezo wa mashindano ya klabu bingwa Afrika, Simba Sc wataingia dimbani kuwakabiri Klabu ya Vipers kutoka Uganda kesho Machi,7 2023 katika dimba la Benjamin  mkapa jijini Dar es salaam saa moja usiku.

Kama klabu pekee kutoka Tanzania inayoshiriki mashindano hayo, Simba Imeeleza maandalizi yake kuelekea mchezo huo, leo katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Akizungumza kocha mkuu wa Klabu hiyo Robert Oliveria ‘Robertinho’ amesema yeye kama kocha amewaandaa vyema vijana wake kimwili na kiakili kwa kuwakabili Wapinzani wao ‘Vipers’.

“Nimewaandaa vizuri vijana wangu kuelekea mechi ya kesho, alama tatu zitabaki nyumbani kama vijana watafata maelekezo niliyowapa katika viwanja vya mazoezi”. Amesema Robertinho.

Nae Beki wa kulia wa simba Sc Shomari Kapombe amesema kuwa wao kama wachezaji wamejipanga vizuri na mchezo huo kwani wana hamu kubwa ya kuhakikisha wanachukua alama tatu ili kufikisha alama sita ikiwa ni sehemu ya kuwapa uhakika wa kutinga hatua ya robo fainali.

“ Huu ni mchezo wetu muhimu wa kutafuta alama tatu zitakzotusaidia kutinga hatua ya robo fainali,hivyo sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri kuwakabili wapinzani wetu”. Amesema Kapombe.

Mechi ya mwisho  ya mashindano hayo, Simba walicheza na Vipers na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika uwanja wa ugenini St Mary’s huko Uganda.

Hadi sasa Simba Sc imeshacheza mechi tatu za klabu bingwa Afrika, ambapo wamepoteza mechi mbili na kushinda mechi moja wakiwa na  umiliki wa Alama tatu katika kundi lao lenye timu nne.

By Jamhuri