Zitalia sana! Nikukumbushe kwanza. Kikao cha Kamati ya Uongozi cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kimeridhia baada ya siku 30 pale serikali itakaporuhusu michezo kuendelea, mechi za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zitachezwa bila watazamaji ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.

Aliyasema hayo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo, mara baada ya kikao ambacho pia kilihudhuriwa na Rais wa TFF, Wallace Karia.

Kasongo aliongeza kuwa kabla ya kuanza kwa ligi hizo, wachezaji wote watafanyiwa vipimo maalumu kuchunguzwa afya zao endapo wameaambukizwa virusi vya corona au la.

Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ilisitisha mwendelezo wa masuala yote ya michezo na mikusanyiko isiyo ya lazima ili kupambana na kasi ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Ila azimio hilo la Bodi ya Ligi ambalo liliridhiwa na TFF limeonekana mwiba mchungu kwa Simba na Yanga ambazo ‘akili zao hazipo katika dunia ya sasa’.

Klabu hizo kongwe zimedai uamuzi huo umetolewa kwa haraka kabla ya kusubiri taarifa za maendeleo ya kuhusiana na hali ya maambukizi ya virusi vya corona.

Simba

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Crescentius Magori, alidai uamuzi huo ulitolewa kwa makosa na Bodi ya Ligi ilipaswa kusubiri kupokea taarifa kuhusiana na hali ya maambukizi baada ya kupita wiki mbili au tatu.

Magori alidai kutangaza kuendelea na mechi za ligi bila mashabiki kwa sasa haikuwa sahihi kwa sababu huenda hali ya maambukizi inaweza kuwa mbaya zaidi, hivyo kuathiri wachezaji na viongozi watakaosimamia michezo hiyo.

“Ni uamuzi wa haraka, hauwezi kujua huko mbele hali itakuwaje, huenda ikadhibitiwa mapema na hali ikarejea sawasawa au hali ikawa mbaya zaidi hata kuchezwa bila mashabiki haiwezekani, nashauri tathmini ingefanyika kuanzia wiki ya tatu baada ya tamko la kusimamisha ligi,” alisema Magori.

Yanga

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alidai uamuzi huo uliotangazwa na Bodi ya Ligi si sahihi na si suluhisho kwa tishio lililopo la ugonjwa huo ambao unaisumbua dunia kwa sasa.

Mwakalebela alisema TFF na vyombo vyake wanapaswa kuwa na subira kwa sababu endapo virusi vya corona vitaendelea kuwapo, itakuwa vigumu kudhibiti mkusanyiko wa mashabiki kwenye ‘vibanda umiza’ ambavyo vimeenea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Bado haitakuwa suluhisho, mkusanyiko wa watu utaendelea kuwapo, hatuna uwezo wa kudhibiti katika maeneo mbalimbali nchini ambayo yatakusanya mashabiki, ni bora tusubiri janga limalizike, huko duniani (nchi zilizoendelea), wameona haina tija, iweje sisi tucheze,” Mwakalebela alisema.

Lazima walie

Wanazunguka tu, lakini ukweli ni kwamba wanajua kucheza bila mashabiki wataumia mno. Hawana vyanzo vya mapato zaidi ya kutegemea aina moja tu ya kitega uchumi – mapato ya mlangoni.

Hata mchezaji wa zamani aliyepata kuwika, Ally Mayayi, anakiri hili, ambapo alisema mechi za Ligi Kuu Bara kuchezwa bila mashabiki zitakuwa na madhara kiuchumi kwa klabu zote zinazoshiriki ligi hiyo.

Mayayi alisema klabu zote zinategemea kujiendesha kwa kutegemea mapato ya milangoni, hivyo kuchukua uamuzi huo kutazifanya timu kuyumba.

“Kwanza ligi kusimama kwa siku 30 kuna madhara makubwa sana, kutafanya viwango vya wachezaji kushuka, upo uwezekano mkubwa wachezaji wakarejea wakiwa hawako fiti, hii italeta matatizo na kuzalisha matokeo yasiyotarajiwa.

“Hata bajeti zilizopo kwa klabu zimekuwa hazitoshi, ligi itakapokuwa imesimama ni wazi kutakuwa na gharama ambazo zitakuwapo, kuna klabu zimekuwa zinapata tabu hata ya usafiri na malazi, klabu zitazalisha madeni mapya, malimbikizo ya posho kama ambayo tumekuwa tukisikia malalamiko ya kudai mishahara.”

Liwe funzo kwao

Chukulia mfano tu wa timu ya Borussia Monchengladbach ya Ujerumani, ambayo imewatamkia wazi wachezaji wake wakae mezani upya na kupanga mishahara yao, vipi kwa Simba na Yanga zisizojipanga?

Mkurugenzi Mtendaji wa timu hiyo, Stephan Schippers, alisema wachezaji wanajua kinachoendelea na wanapaswa kupunguza mishahara ila hawatakufa njaa.

Wakati wana wadhamini wengi, Borussia imekuwa timu ya kwanza Ujerumani kuamua hilo na tayari mkurugenzi huyo na Kocha Marco Rose wamejipunguzia mishahara.

Wasiojipanga watayumba

Prof. Christoph Breuer kutoka Taasisi ya Uchumi na Utawala wa Michezo  katika Chuo Kikuu cha Michezo kilichopo Cologne, Ujerumani, amekiri mzimu umeikumba michezo na watu pekee wanaotakiwa kulijibu hili ‘ni madaktari pekee’.

“Kucheza bila watazamaji ni pigo kubwa, pia wadhamini wengi kuanzia haki za televisheni na matangazo watajitoa, lakini kama timu hazikujipanga zitaathirika zaidi.

“Nazisikitikia hasa timu za Afrika, ambao wengi wanategemea mapato ya milangoni, ila hili pia liwe funzo kwao, kwani kuna vyanzo vingi vya mapato.”

Zifanye nini?

Kama alivyosema Profesa Christoph Breuer, klabu kama Simba na Yanga zinashangaza kulia wakati huu, wakati zilipaswa ziwe na mabadiliko makubwa kuanzia huko nyuma.

Huu ni wakati wa watu wa masoko kujitafakari zaidi na kujua kile wanachopaswa kufanya, kwani hakuna anayejua virusi hivi vya corona vitadhibitiwa lini.

Mungu tu atunusuru, ila Simba na Yanga lazima wajitafakari.

1107 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!