Mpira wa miguu ni mchezo wenye mambo mengi sana. Ndiyo maana soka ina a.k.a nyingi kama Koffie Olomide. Yeye ni Grand Mopao, Papa Fololo, Gangi ya Film, Le Jeune Pato, Quadra Koraman, Songe ya Mbeli, Le Grand Mbakala, Papa Rocky, Le Guide le Prophete, Petit ya Yesu, Decennie, Papa Sucre, Soso ameli Ngandu.

 Nimezitaja chache kati ya a.k.a 39 alizonazo. Jina lake la kwenye hati ya kusafiria ni Antonie Christopher Agbepa Mumba, hata Koffie Olomide ni jina la kutafutia pesa tu.

Ndivyo ilivyo kwa mchezo wa mpira wa miguu. Nguvu na ukubwa wa mchezo huu uliowafanya kina Ujugu wa Buza kuwaonya nahodha wa Aston Villa aliyepo Uingereza. Kwenye soka aliyekula na asiyekula wote hawasikii njaa. Hata majina yake mengi yanathibitisha ukubwa huo. Soka, kabumbu, kandanda, gozi la ng’ombe, mtanange nk.

Soka imeua watu, kandanda limewapa watu vilema, kabumbu inawapa watu utajiri, kabumbu imewafilisi watu, mpaka waganga wa kienyeji wanafaidika na gozi la ng’ombe.

Nguvu ya soka ilisimamisha vita Nigeria mwaka 1967 kumpisha Pele. Pande mbili zinazopigana zilikubaliana kusimamisha mapigano kwa saa 48  kuupisha mchezo huo wa hisani ambao Pele alicheza. Soka hufanya aliyekula dagaa na aliyekula kuku wote wafurahie maisha.

Watu 300 nchini Peru  walifariki dunia mwaka 1964 baada ya mwamuzi wa mchezo kupokea simu akiwa uwanjani akichezesha. Mwaka 1998 Wachezaji 11 wa timu moja nchini Kongo walifariki dunia baada ya  kupigwa na radi wakati wa mechi. Soka inasisimua, soka inakera, soka inaliwaza, soka inaumiza.

Soka inaua penye huruma, huleta kisasi pa kusamehe.

Kwa muda nrefu watu walijadili kilichotokea kati ya mechi ya Yanga dhidi ya Lipuli wakati golikipa Metacha Mnata alipoudaka mpira kwenye mlingoti wa goli. Mpira huo ulizusha mjadala iwapo ulivuka mstari wa goli au la. Cha kushangaza, mwamuzi msaidizi akasema hiyo ni kona!

Sheria hiyo inasema goli litahesabiwa halali ikiwa mpira wote utavuka mstari wa goli, ilimradi usiwepo ukiukwaji wa sheria kama kuzidi kwa mchezaji, mchezaji kuchezewa vibaya au kushika mpira. Iwe mpira ulivuka au la, mjadala ulizushwa na uamuzi wa mwamuzi, kwa nini ni kona?

Mimi ni mmoja ya watu ninaoamini kwamba kama kuna timu zinahonga waamuzi, basi ni mara chache sana. Ukweli ni kwamba waamuzi wengi nchini wana viwango duni vya kuchezesha. Kitaalamu mechi inayochezeshwa na mwamuzi mbovu timu itakayofaidika na ubovu wake ni ile itakayokaa na mpira muda mrefu zaidi wakati wa mchezo.

Simba ukiacha mechi na Lipuli kipindi cha kwanza, ndiyo timu ambayo katika mechi zake hata  ikifungwa huongoza kwa umuliki wa mpira. Katika utando huu wa makosa ya waamuzi lazima ifaidike. Siamini kama wananunua.

Ilikuwa hivi hivi kwa Barcelona ya Gardiola, ikawa hivi kwa Manchester ya Alex Ferguson, siku si nyingi Liverpool nayo ikaingia kwenye orodha hiyo.

Pia kuna mtu anaitwa Metacha Mnata anafaidika mno na vituko vya mwamuzi. Kama mechi ile dhidi ya Lipuli ingeisha kwa 2-2 au Yanga kushinda 2-1 na kusingekuwa na vituko vya mwamuzi, mjadala ungekuwa kiwango kibovu kilichoonyeshwa na golikipa huyu wa timu ya taifa.

Mipira yote miwili  (ule uliopigwa na Davis Mwasha Dk 54 na ule uliozua utata), haikuwa mipira ya golikipa mwenye hadhi ya timu ya taifa kufungwa au kutuletea mjadala.

Hata huu mjadala wa goli au si goli uliletwa na ubovu wa Metacha. Mpira aliopigiwa haukuwa na hatari yoyote ile, alikuwa peke yake, hakukua na sababu yoyote ile ya kutetemeka kwa kiwango kile. Goli lililokubaliwa pia ni sehemu ya udhaifu wake. Aliwapanga mabeki kwenye faulo kisha akakaa nyuma yao.

Dunia haina golikipa anayekaa nyuma ya ukuta wake wakati wa faulo. Kipa akipanga ukuta kushoto hukaa kulia, kadhalika akipanga kulia hukaa kushoto, hii ndiyo sababu faulo yoyote ile ikivuka ukuta, asilimia 85 huwa ni goli.

Nguvu ya matukio katika soka imemnusuru Metacha. Leo hayupo anayejadili udhaifu wake, wote tunapiga kelele kwa kikichotokea. Maajabu ya vituko vya soka vimemuacha Metacha salama, vinginevyo kwa makosa aliyoyaonyesha dhidi ya Lipuli angekuwa katika wakati mgumu.

Hili ndilo soka, kabumbu, kandanda. Ndio mchezo unaofanya kwa sababu ya ushabiki profesa wa Chuo Kikuu akafanana na asiyekwenda shule kabisa. Ndio mchezo ambao ukiandika ukweli unaowachoma Simba, Yanga watakusifia na Simba watakutukana, ndiyo sehemu pekee ukimsifia Morrison kwa bao alilofunga dhidi ya Lipuli, Simba watakutukana na Yanga watasema “kaka wewe unajua sana.” Una nguvu hata wengine wanakaribia kuupa hadhi ya dini zao.

Maoni na ushauri

0629500908

nnnguzo@gmail.com

1504 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!