Mabingwa wa Tanzania, Yanga SC wametupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelodi Sundowns kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku huu Uwanja wa Loftus Versfeld Jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Katika mchezo huo wa marudiano wa Robo Fainali, Refa Dahane Beida wa Mauritania alilazimika kutumia Teknolojia ya VAR dakika ya 58 kuamua juu ya shuti la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mburkinabe, Stephane Aziz Ki lililoonekana kudundia ndani ya mstari wa lango si bao.

Katika mikwaju ya penalti waliofunga za Mamelodi Sundowns ni viungo Mchile, Marcelo Allende, Mbrazil Lucas Ribeiro Costa na mzawa, Neo Maema wakati ya nyota kutoka Uruguay, Leandro Sirino iliokolewa na kipa Mmali, Djigui Diarra wa Yanga.

Waliofunga penalti za Yanga ni winga Mghana, Augustine Okrah na mshambuliaji wa Ivory Coast, Joseph Guédé Gnadou huku Aziz Ki na mabeki Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wakikosa.

Ikumbukwe mechi ya kwanza ya Robó Fainali Jumamosi iliyopita timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana pia Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Sasa Mamelodi Sundowns itakutana na mshindi wa jumla katí ya Esperance ya Tunisia na ASEC Mimosas ya Ivory Coast zinazorudiana kesho baada ya sare ya 0-0 pia kwenye mechi ya kwanza.

Katika mchezo mwengine Simba SC kwa mara nyingine imetupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika Hatua ya Robó Fainali baada ya kufungwa 2-0 na wenyeji, Al Ahly usiku huu Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo nchini Misri.

Mabao yaliyoizamisha Simba leo yamefungwa na kiungo mzawa, Amr El Soleya dakika ya 47 akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji Mfaransa, Anthony Mbu Agogo Modeste na mshambuliaji mzawa, Mahmoud Abdelhamid Soliman dakika ya 90na ushei.

Kwa matokeo hayo Al Ahly inakwenda Nusu Fainali kwa ushindi wa jumla wa 3-0 kufuatia kushinda 1-0 pia kwenye mchezo wa kwanza Ijumaa iliyopita Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Sasa Mabingwa hao watetezi, Al Ahly na watamenyana na mshindi kati ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Petro de Luanda ya Angola katika Nusu Fainali, ambao mechi ya kwanza zilitoka sare ya 0-0 Jijini Lubumbashi.

By Jamhuri