Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Songwe

Mkoa wa Songwe unakabiliwa na uhaba wa nishati ya mafuta ya petrol na dizeli na kuzua hofu kwa watumiaji wa vyombo vya moto wakihisi huenda yakaadimika na kusababisha usumbufu.

Uhaba huo wa mafuta umeanza kujitokeza siku tano zilizopita ambapo vituo mbalimbali katika miji ya Vwawa na Mlowo vikidai kukosa kabisa bidhaa hiyo, huku katika mji wa mpakani wa Tunduma vituo vichache vikionekana kuuza nishati hiyo.

Baadhi ya madereva wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa nishati hizo wamejikuta wakilazimika kuondosha magari yao baada ya kuambiwa na wahudumu kuwa hakuna nishati hiyo, huku walanguzi nao wakitumia fursa hiyo kuuza mafuta kwa bei ya kuruka ya shilingi 4000 hadi 5000 kwa lita tofauti na bei elekezi ya serikali ya shilingi 2853 kwa petrol na shilingi 2660 kwa dizeli kwa mkoa wa Songwe.

Mmoja wa waathirika wa kukosekana kwa mafuta,Mchungaji Haile Mwaijumba, Mkazi wa Ihanda, Wilayani Mbozi, akiwa na gari yake ndogo katika moja ya kituo cha mafuta alisema tatizo hilo la kukosekana kwa nishati ya mafuta limeleta sumbufu mkubwa na limejitokeza bila kupewa taarifa.

Kwa upande wake,dereva Bodaboda alionekana kushangaza na vituo vya mafuta katika Mkoa wa Songwe kukosa mafuta wakati juzi tuu serikali ilitangaza kushusha bei ya bidhaa hizo za mafuta.

Alisema hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa na watalazimika kusitisha biashara ya kubeba abiria kama hali ya kukosekana mafuta itaendelea kwa muda mrefu katika mkoa wa Songwe.

Mmoja wa wauzaji mafuta ambaye ni msimamizi wa kituo cha kuuza mafuta cha Manyanya mjini Vwawa, Wilayani Mbozi, alisema tatizo hilo limekuwa likijirudia kila mwaka inapofika miezi hii, huku akianisha kuwa kwa sasa waauzaji wa mafuta wananunua kwenye ‘Depo’ mmoja tuu iliopo Jijini Dar es Salaam.

“Naomba watu wajue kuwa tatizo si wafanyabiashara au matajiri zetu bali sijui tatizo ni nini kwani kila mwaka ikifika miezi kama hii kuna ibuka tatizo la kukosekana kwa mafuta na hivi tunavyozungumza kuna depo moja tuu inayouza mafuta huko Dar es salaam hivyo inakulazimu kukaa muda mrefu kwenye foleni kupata mafuta” alisema Ringa.

Hata hivyo kuadimika kwa mafuta mkoani hapa, kumegeuka fursa ambapo baadhi ya watu wameanza kuuza mafuta hayo kwa bei ya kulangua, ambapo wanauza lita moja ya petrol na dizeli kwa shilingi kati ya 4,000 hadi 5,000 ukilinganisha na bei elekezi ya serikali iliyopo kwenye vituo rasmi ya shilingi 2853 kwa petrol na shilingi 2660 kwa dizeli kwa mkoa wa Songwe.

Mmoja wa walanguzi hao, Jackson Haonga, alisema amelazika kuuza mafuta hayo kwa bei ya juu baada ya kuona yameadimika na watumiaji wengi wanahangaika kuyapata.

“Mafuta haya ni stock yangu niliyokuwa niikiipeleka kuuza kijijini, lakini baada ya kuona watu wanahangaika sana nimeamua kuuza ili kuwahudumia wenzangu ambao wamekuwa wakihangaika” alisema Haonga.

By Jamhuri