Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Benki ya Stanbic Tanzania imesema maboresho ya hivi karibuni katika soko la mitaji nchini yamefungua fursa mpya kwa taasisi za umma kupata fedha za muda mrefu kwa ajili ya kugharamia miradi ya kimkakati.
Benki hiyo imetoa kauli hiyo wakati wa Mkutano wa Nne wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026, ulioanza Jumatatu jijini Arusha.
Zaidi ya wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wakuu 700 wa taasisi za umma wanashiriki katika mkutano huo wenye kaulimbiu, “Mashirika ya Umma Yenye Ufanisi wa Juu kwa Uchumi Shindani, Shirikishi na Imara katika Kutekeleza Dira 2050.”
Chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imechukua hatua mbalimbali mwaka huu katika kuimarisha masoko yake ya fedha.
Mwezi Agosti mwaka huu, Benki Kuu ya Tanzania ilitangaza kuwa hati fungani za muda mfupi na hati fungani za Serikali, ambazo awali zilikuwa wazi kwa wawekezaji wa Kitanzania, sasa zimefunguliwa pia kwa wawekezaji wa kigeni.
Aidha, Serikali imetangaza mipango ya taasisi za umma kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua itakayowapa Watanzania fursa ya kumiliki hisa katika taasisi zinazowahudumia.
“Maboresho ya Serikali yanajenga mazingira imara zaidi kwa uwekezaji na mitaji ya muda mrefu. Kama taasisi za kifedha, jukumu letu ni kuleta utaalamu wetu, mitandao yetu na uwezo wetu wa kifedha sambamba na azma hiyo ya Taifa. Tupo tayari kushirikiana na Serikali katika kuitekeleza,” alisema Elias Ngunangwa, Mkuu wa Mahusiano na Wateja Wakubwa wa Stanbic Bank.
Ngunangwa alisema Dira 2050 imeweka azma ya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati cha juu na kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, akisisitiza kuwa taasisi za umma zina nafasi muhimu katika kufanikisha azma hiyo.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Stanbic imesema imetoa zaidi ya dola za Marekani bilioni moja katika ufadhili wa maendeleo nchini Tanzania, ukiwemo kwa ajili ya miradi ya miundombinu, nishati na biashara.
Euromoney imeitaja Stanbic kuwa Benki Bora ya Uwekezaji Tanzania kwa miaka sita mfululizo, huku Soko la Hisa la Dar es Salaam hapo awali likiitambua kama benki bora ya huduma za uhifadhi wa dhamana.
Ikiwa sehemu ya Standard Bank Group, Stanbic inaunganisha taasisi za Tanzania na mitaji pamoja na utaalamu kutoka Afrika na maeneo mengine duniani.
Stanbic imesema itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Soko la Hisa la Dar es Salaam pamoja na taasisi za umma, katika kusaidia hatua inayofuata ya maendeleo ya soko la mitaji nchini.
Benki hiyo ni miongoni mwa wadhamini wa mkutano huo ambao utaendelea hadi Jumatano, Septemba 30, 2026.











