JUBA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezipa muda wa mwezi mmoja pande hasimu zinazogombana nchini Sudan Kusini kufikia makubaliano vinginevyo nchi hiyo ijiandae kukabiliana na vikwazo.

Mchakato huo uliongozwa na Marekani ndani ya Umoja huo ulipata ushindi mdogo wa kura 9 katika baraza hilo lenye nchi wanachama 15 na huku kukionekana na kuwepo kwa hali ya ubishani miongoni mwa wanachama.

Wakati azimio hilo likipitishwa nchi nyingine za China, Urusi na Ethiopia ambazo ni washirika muhimu katika juhudi za kutafuta amani ya eneo hilo hazikupiga kura wakati wa uamuzi huo na kuacha maswali.

Nchi za Ethiopia na Guinea ya Ekweta hazikupiga kupiga kura huku zikisema kuwa ni sharti juhudi za amani zikapewa nafasi zaidi, wakati huo huo Cote Di’Voire, ambayo ni nchi ya tatu ya Afrika katika baraza hilo iliunga mkono azimio hilo.

Azimio hilo limemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kuwasilisha ripoti juu ya mgogoro huo ifikapo Juni 30, kueleza ikiwa makubaliano yaliyofikiwa Disemba mwaka jana yanatekelezwa na pande husika.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley ameliambia baraza hilo kuwa Marekani imepoteza subira na uvumilivu juu ya mgogoro huo unaoendelea kuwaathiri akina mama na watoto.

Tayari Marekani imeorodhesha majina ya maafisa sita toka nchini humo wanaoweza kujikuta wakikabiliwa na vikwazo vya kusafiri na kutafishwa kwa mali zao, uamuzi ambao utatolewa na Baraza la Usalama la Umoja huo.

Balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa, Akuel Bona amesema azimio la kuwawekea vikwazo maafisa wa nchi yake si sawa na huenda lisichangie chochote kukabiliana na matatizo nchini humo.

Mchakato wa amani wa Sudan Kusini kwa sasa umefikia hatua muhimu na kuongeza kuwa kuna matumaini na uwezekano wa kurejea kwa hali ya amani nchini humo ni mkubwa.

Baadhi ya maafisa wanaolengwa kuwekewa vikwazo ni pamoja na Waziri wa Ulinzi, Kuol Manyang Juuk kwa kuongoza mashambulizi Kaskazini Mashariki mwa mji wa Pagak ambao ulikamatwa na waasi mwaka 2017.

Wengine ni Kaimu Waziri wa mambo ya Nje, Martina Elia Lomuro kwa kutishia vyombo vya habari, kuzuia misaada ya kiutu na kuhujumu kazi ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini.

Pia Waziri wa Habari Michael Makuel ametajwa kwa madai ya kuhusika katika kupanga shambulizi katika kambi ya Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2014.

Balozi wa Ethiopia Umoja wa Mataifa, Tekeda Alemu ameonya hatua ya kuweka vikwazo inaweza kupelekea kuvunjika kwa juhudi za amani za kanda hiyo zinazoongozwa na jumuiya ya ushirikiano wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika- IGAD.

By Jamhuri