Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Shule ya The Madrasat and Masjid Nnuru Sotele iliyopo wilayani Mkuranga wameiomba serikali kuzichunguza akaunti za fedha za taasisi ya wataalamu wa Kiislamu nchini, TAMPRO, ili kubaini usahihi wa akaunti hizo.

Wajumbe wa Bodi ya Jumuiya ya The Madrasat and Masjid Nnuru Sotele wanaituhumu TAMPRO kwa kutumia  jina la Shule ya Sekondari Sotele kuomba misaada kwa wahisani mbalimbali na kuzitumia fedha hizo kwa malengo yao binafsi.

Awali, shule hiyo ilimilikiwa na Jumuiya ya The Madrasat and Masjid Nnuru Sotele lakini baadaye ukafanyika mkakati umiliki wake ukahamishwa kwenda kwa taasisi ya TAMPRO.

Pia TAMPRO wanatuhumiwa na jumuiya hiyo kwa ukwepaji wa kodi kwa miaka mingi ikidaiwa kuwa tangu mwaka 2006 walipotwaa umiliki na kuanza kuiendesha shule hiyo hawajalipa kodi.

Wadhamini hao wanadai kuwa kwa sababu wao ndio wanaotambulika kisheria, serikali imewaandikia wao wakitakiwa na serikali kulipa kodi hiyo kwa kipindi chote hicho.

Pamoja na tuhuma hizo, The Madrasat and Masjid Nnuru Sotele wanaiomba serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi iwarudishie umiliki wa Shule ya Sekondari Sotele ili waiendeshe wenyewe.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mwenyekiti wa bodi ya jumuiya hiyo, Miraji Jongo, anasema wana mikakati ya kuirejesha shule hiyo katika hadhi yake ya zamani iwapo watakabidhiwa waiendeshe.

Anasema kabla ya kuingia migogoro baina yao na taasisi ya TAMPRO shule hiyo ilikuwa kwenye hali nzuri na ilikuwa na mwitikio mkubwa wa kupokea wanafunzi.

“Wakati tunaingia makubaliano na TAMPRO miaka ya 2000 shule ilikuwa na wanafunzi 60, leo tunavyozungumza shule imebaki na wanafunzi wachache kuliko idadi tuliyoanza nayo,” anasema Jongo.

Anaeleza kuwa pamoja na hali ya shule hiyo kuwa mbaya, TAMPRO wanaing’ang’ania ilhali hawaiendelezi ipasavyo.

Aidha, anadai kuwa mwaka 2005 TAMPRO walijimilikisha kinyemela eneo la shule hiyo lenye ukubwa wa hekta 7.46 wakati eneo hilo linatambulika kama miliki ya jumuiya.

Jongo ameishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwarejeshea umiliki wa eneo la mita za mraba 23,944 walilokuwa wamenyang’anywa kinyemela na TAMPRO.

“Eneo letu lilipimwa kwa ujumla na TAMPRO na kusajiliwa mwaka 2005 bila kutushirikisha wakapewa namba 40467 kisha wakajimilikisha kinyemela kwa barua yenye kumb. Na. LD/MK/991/6 JBM ya Julai 22, mwaka huo,” anasema Jongo.

Aidha, anasema mwaka 2012 TAMPRO waliandika barua yenye kumb. Na. TAMP/ge/01/05/2012 kwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa ajili ya kubadili umiliki wa shule hiyo.

Hali hiyo imesababisha uongozi wa The Madrasat and Masjid Nnuru Sotele mwaka 2018 kuvunja mkataba wa TAMPRO wa kuendelea kuendesha shule hiyo hali iliyowafanya wakimbilie mahakamani.

TAMPRO walifungua kesi mahakamani, shauri namba 1 la mwaka 2019 wakidai kulipwa Sh bilioni 2.1, lakini mahakama ikatupilia mbali shauri hilo.

Hata hivyo Mwenyekiti wa TAMPRO, Hashimu Saiboko, amelieleza gazeti hili kuwa waliingia mkataba wa kuendesha shule hiyo mwaka 2006 lakini Jumuiya ya The Madrasat and Masjid Nnuru Sotele wakawa hawatoi ushirikiano.

Anaongeza kuwa hawezi kuzitolea ufafanuzi tuhuma za kuitumia Shule ya Sotele kuombea misada kwani wakati zinasemwa na wajumbe wa bodi hiyo yeye hakuwepo.

Anadai wajumbe wa bodi ya jumuiya hiyo hawakutakiwa kwenda kwenye vyombo vya habari baadala yake wangeiomba mahakama iliyohukumu kesi iwape amri ya kutekeleza hukumu kama wameshinda kesi.

“Mimi sikuwepo wakati wanaongea na nyinyi, hayo mambo ya kusema kuwa sisi tunaitumia shule kuombea misaada siyafahamu na sitayaongelea. Nafikiri hawajui kama wameshinda kesi au hawajashinda, wanachotakiwa kufanya ni kuiomba mahakama ya Kibaha iliyohukumu kesi iwape amri ya kutekeleza hukumu,” anasema Saiboko.

By Jamhuri