Kampuni ya Neelkanth Salt Limited imetoa msaada wa viti 100 na katoni 300 za chumvi kwa Shule ya Sekondari Shungubweni kama hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu mitihani yao ya darasa la saba mwaka jana wanajiunga na kidato cha kwanza.

Mkurugenzii Mkuu wa kampuni hiyo, Ahmed Said, anasema jitihada za serikali za kutaka wanafunzi wote waanze kidato cha kwanza pamoja ni muhimu kuungwa mkono ili kuwafanya wanafunzi kujiona kuwa ni wamoja.

Ameyataka mashirika, kampuni, taasisi na hata watu binafsi kuunga mkono jitihada hizo za serikali kwa kutoa misaada ya vifaa na ujenzi wa miundombinu ili kuwawezesha wanafunzi hao kusoma katika mazingira bora.

“Sisi tumetoa vifaa hivi kwa shule hii ya wasichana ili viwasaidie katika masomo yao,” anasema.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Yusuf Selemani, ameishukuru kampuni hiyo kwa msaada wake.

Anasema kabla ya msaada huo walikuwa wanahitaji viti 250 na meza 200.

Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 600, ambapo kati yao 250 wameanza kidato cha kwanza mwaka huu.

Wakati huo huo, wazazi ambao watoto wao wamefaulu mitihani ya darasa la saba mwaka jana wametakiwa kuhakikisha wanawapeleka watoto wao katika shule za sekondari walizopangiwa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mshamu Munde, wakati akizungumza na JAMHURI.

Anawataka wazazi kuacha visingizio ili kukwepa kuwapeleka watoto wao shuleni, kwani elimu ni muhimu kwao na kwa taifa.

Anasema tayari halmashauri imekwisha kuboresha miundombinu na vifaa vipo vya kutosha, hivyo hakuna kisingizio kwa wazazi kushindwa kuwapeleka watoto wao shuleni.

“Hata kama kuna changamoto katika baadhi ya sehemu, hiyo isiwe sababu ya wazazi kuacha kuwapeleka shuleni watoto wao, kwa sababu serikali inashughulikia changamoto hizo,” anasema.

457 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!