Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Kuelekea siku ya wanawake duniani inayoadhimishwa kila mwaka Machi 8,Taasisi isiyo ya Kiserikali inalojihusisha na masuala ya Wanawake nchini ya Dira Women(DIWO )imewakutanisha wanawake wa Mkoa wa Dodoma katika usiku wa mwanamke, uchumi na familia ili kuwaleta pamoja na kuwajenga kiuchumi na kifamilia.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo (DIWO) Shamsa Danga ametumia nafasi hiyo kuwataka wanawake kushirikiana na kusimama imara katika kuhakikisha wanafanya kazi zote bila ya kujali jinsia zao ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Akizungumza jana Machi 2,2024 jijini hapa mesema hakuna kazi maalumu za wanaume wala kazi maalumu za wanawake na kwamba ni lazima kuwa imara na kukubali kuwa kazi zote zinafanywa na kila mtu.

Amesema Serikali ilipoamua kumuinua mwanamke katika ngazi mbalimbali sio kama imekosea, bali inataka wanawake waweze kujitegemea kwa kujiajiri wao wenyewe bila ya kusubiri ajira kutoka Serikalini.

“Wanawake shikamaneni,lazima tukubali kuungana na kushirikiana kuona kila penye mwanamke tunahakikisha anafanikiwa,hatupaswi kiwekeana choyo wala roho mbaya, kwani umoja wetu ndiyo silaha ya mafanikio, ” Amesema

Naye Kamishna Msaidizi wa Idara ya maendeleo ya Sekta ya fedha Wizara ya fedha Janeth Lewis Hiza amesema ili kujenga uchumi lazima mwanamke akukubali kushaurika na kukubali kujifunza kwa waliofanikiwa.

Amesema changamoto ya matumizi mabaya ya muda zinapaswa kuepukika ili Mambo yaende huku akitolea mfano kuwa kuna baadhi ya Wanawake hutumia muda mwingi kwenye simu bila faida na kujikuta wakipoteza.

“Lazima ujue unafaidikaje na simu tangu umeanza kuitumia,niwashauri tu kuwa inahitaji ujasiri lazima uwe na maamuzi magumu ili ufaulu,mama hata kama huna mtoto wewe ni mama unaweza kuwa umuhimu kwa wanawake wengine na ukawa mlezi kwa watoto wengine

Akizungumza katika tukio hilo amesema wanawake wanapaswa kuwa nguvu moja ili kuendelea kulinda hadhi na heshima ya waasisi wanawake akiwemo Bibi Titi Mohamed ambapo kwa namna moja au nyingine walipigania nguvu na umoja wa wanawake

Kuhusu masuala ya uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa amesema ili kuweka usawa lazima wanawake bila kusita wajitokeze kikamilifu kushiriki kugombea katika nafasi mbalimbali ili kupata nafasi ya kujipambania na kumaliza matatizo yao.

Mbali na hayo amesema wanawake bado wana jukumu la kuwalea watoto na vijana kutokana na kuingia mdudu mmomonyoko wa maadili hivyo kwa kuongeza ukaribu wa kuzungumza Mara kwa Mara na watoto wanaweza kuwa katika maadili yanayotakiwa.

Kwa upande wake Mhadhiri wa chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM)Dk. Deograsia Nduguru amezungumzia ukombozi wa mwanamke kifikra ambapo ameeleza kuwa mwanamke ana nchango mkubwa na kuendeleza amani mwanamke anapaswa kuhishughulisha katika uzalishaji na afya na kwamba familia inaweza kukua kiuchumi ikiwa msingi wa uzalishaji utapewa kipaumbele kwa kuzingatia malezi na elimu kwa watoto.

“Ili kukua kiuchumi wanawake waachane na fikra potofu zozote zinazokwamisha maendeleo kiuchumi,Kuwa na fikra bunifu kwenye jamii mpya na kuepukana na changamoto zilizopo kwenye jamii itawasadia,tunatakiwa kupewa hadhi tunayostahili, mwanamke bunifu huweza kujipambanua na kujiweka katika nafasi , mkono uleao mwana ndio uleao taifa,” amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP-Mtandao Lilian Liundi amewaeleza wanawake hao kuhusu umuhimu wa bajeti yenye mtizamo wa kijinsia na kufafanua kuwa bajeti hiyo ni lazima izingatie uchambuzi wa hali halisi ya makundi tofauti katika jamii kwa kuzingatia jinsi na rika kulingana na mahitaji.

Ameeleza kuwa bajeti nyingi zinatengenezwa lakini hazina jicho la kina la uchambuzi wa vigezo vya kijinsia kwa sababu haizingatii mahitaji ya watu wenye ulemavu na makundi mengine maalumu.

“Bajeti nyingi hupangwa bila kuzingatia mlengo wa kijinsia, mfano wajawazito lishe yao ni tofauti na mtu wa kawaida, anayenyonyesha pia lishe inahitaji bajeti lakini mara ngapi familia wanajadili bajeti ,lazima wanafakilia kujadili hatua za bajeti ya kijinsia kwa kuweka vipaumbele vya mahitaji kulingana na kipato na baadae utekelezaji kwa kuzingatia matokeo tarajiwa ili kujua mapungufu na maboresho zaidi, “amesema

Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo wa TGNP amesisitiza kuwa ,” Ni muhimu kuzungumzia maendeleo kwa kuhusisha na bajeti ya ngazi ya familia,kipato cha familia kikoje nani anachangia kipato hicho,Kuna kipato huduma ambacho hufanywa na mwanamke ambapo mara nyingi watu wahakihesabu,ifike wakati tusaminishe kipato huduma anachofanya mwanamke kuwa ni sawa na ujira mkubwa anaolipwa mtu, “amesiaitiza

Anafafanua kuwa, ” Kazi anazofanya mwanamke ni nyingi,ukiwekwa pale mzani utagundua mama anafanya kazi kubwa
angalau badala ya kutumia mkaa na kuni basi gesi iwepo,malengo na mafanikio ya nchi hayafiki panapotakiwa kwa sababu mipango mingi haizingatii mahitaji ya ngazi ya familia,sisi wanawake tuna nafasi twende pamoja tusiachane, “amesema

By Jamhuri