Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

Taasisi ya Miriam Odemba ‘Miriam Odemba Foundation’ yenye makao yake Jijini Dar-eS-Salaam inatarajia kujenga matundu zaidi ya 40 kwenye shule ya Msingi Mwendapole pamoja na kukarabati jengo chakavu linalosomewa na watoto wa elimu ya awali .

Msaada huo unakwenda kusaidia kwani utaondoa changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo 43 ambayo yanahitajika kwani yaliyopo ni matuu pekee hali inayohofiwa maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo UTI.

Hayo yalielezwa na msemaji wa taasisi kwa niaba ya Miriam Odemba alipofika kuitembelea shule hiyo kupata taswira halisi ya uhitaji na gharama zake.

Akiwasilisha taarifa ya uhitaji, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Rajabu Chalamila alisema kuwa jumla ya wanafunzi waliopo ni 1004 wanaotumia matundu matatu tu wakiwemo watoto 90 wa Elimu ya awali (chekechea).

Aidha, Chalamila ameongeza kuwa katika hali ya Kawaida, Shule ilipaswa kuwa na matundu 46 lakini wanapungukiwa na 43 kwani yaliyopo ni matundu matatu pekee.

Alieleza , nguvu ya haraka inahitajika ili kuwanusuru watoto hao hasa wa kike dhidi ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo UTI.

“Nawashukuru wazazi, Tuliwafuata kuwaomba wameweza kuchangia na kujenga matundu 10 ili kuwawezesha watoto kujisitiri, hata hivyo hayajakamilika na kufanya tatizo kuendelea kuwepo” amesema Chalamila

Akizungumzia upande Walimu, Chalamila alibainisha kuwa nako Kuna changamoto kwani walimu wa kike wapo 21 lakini wanatumia matundu 2 ya Vyoo na kuhatarisha afya zao..

Mwakilishi wa Miriam Odemba Foundation ameishukuru Ofisi ya Mkurugenzi kwa kuwaruhusu kufanya kazi ndani ya Halmashauri ya Mji Kibaha na kwamba wameona uhitaji, wamechukua picha na wataziwasilisha kwa Miriam Odemba ambaye kwa Sasa yupo nchini Ufaransa akiendelea na shughuli zake za uanamitindo

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwendapole Muhidin Mohamed alitoa salaam za Mtaa na kuipongeza taasisi ya Miriam Odemba kwa kuamua kuanza na Shule ya Msingi Mwendapole.