Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

TAASISI isiyo ya kiserikali ya Onastories,kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa, wamezindua maonyesho ya mradi wa uhifadhi wa tamaduni ya Makonde kwa njia ya kidigitali,ambayo kuanza kuonyeshwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo Instagram na facebook kupitia vichujio picha “Instagram filters”, Mradi huo, umezinduliwa jana jioni Oktoba 12, 2023, jijini Dar es Salaam.

Awali Mkurugenzi wa Onastories ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia halisia, Bi.Tulanana Bohela, amesema uzinduzi huo unahusisha mila za kabila la Makonde kutangaza tamaduni zao hasa ‘chale’ za uso pamoja na uchongaji wa vinyago.

“Kwa kuanzia tumewawezesha wabunifu 12 wenye uwezo na maarifa ya teknolojia ya uhalisia ongezi kwaajili ya kuhifadhi utamaduni wa Makonde kidijitali.

“Kuchochea ushirikiano kati ya wahifadhi wa utamaduni, wanahistoria, wakusanyaji wa nyaraka na wabunifu ili kuhakikisha uhalisia unakuwepo.

Kuweka chale ya Makonde katika mfumo wa kidigitali na kuifanya iweze kupatikana kwa kuhifadhi, kuelimisha, na kuunganisha kwenye majukwaa kama vile Instagram, Facebook,na TikTok,” alisisitiza Bohela.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Makumbusho ya Taifa, Bi.Elvida Max, akizungumza wakati wa uzinduzi huo,amesema mpango huo utadumisha tamaduni vizazi vingi vijavyo.

Amebainisha kuwa, kabla ya uzinduzi huo, Onastories imefanya maandalizi kwa miezi sita, kufuatilia namna wamakonde wanavyoishi na kuiweka historia hiyo kwenye mfumo wa kidigitali na baadae kuhifadhiwa makumbusho ya Taifa.

“Mradi huu umechochewa na kupotea kwa tamaduni ya uchanjaji chale katika jamii ya Kimakonde,athari za mabadiliko ya kiteknolojia katika ushawishi wa watalii katika makumbusho, na jinsi teknolojia inavyoweza kutumika kuunganisha kizazi cha leo na yale waliyoyafanya wahenga kwa kutumia teknolojia ya uhalisia wa ongezi”. Amesema Elvida Max.

Nae Mwakilishi Mkazi wa UNESCO, nchini, Michael Toto amepongeza Taasisi ya Onastories na Makumbusho ya Taifa kwa mpango huo wa kutunza tamaduni ya Makonde kwa vizazi vya sasa na baadae.

Aidha,katika tukio hilo wadau na watu mbalimbali wameweza kujionea namna tamaduni ya kabila la Makonde kupitia simu zao za mkononi.