Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umezitaka Taasisi, Mashirikisho na Vyama mbalimbali vya michezo nchini kutumia Miliki Ubunifu kuhakikisha inadhibiti uharamia unaofanyika katika sekta michezo nchini ili kukuza na kuimarisha sekta hiyo.

Wito huo umetolewa leo tarehe 06 Oktoba 2026 na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa wakati akifungua warsha maalumu kwa wadau wa michezo nchini iliyofanyika katika ukumbi wa King Jada Jijini Dar es Salaam ambapo aliwataka pia wadau wa michezo kuongeza uelewa kuhusu namna ya kulinda na kutumia ubunifu kukuza michezo.

“Kimsingi, sioni sababu ya kushindwa kudhibiti jezi feki, skafu feki, beji feki na bendera feki za vilabu vya michezo zinazouzwa pembezoni mwa viwanja vya mpira wakati wa mechi au hata kwenye masoko makubwa kama kariakoo Dar es Salaam. Suala hili lipo ndani ya uwezo wetu kabisa, suluhisho pekee la kudhibiti uharamia huu ni kupitia Miliki Ubunifu na vyombo vy Serikali na wahusika wenyewe” alisema Bw. Nyaisa

Awali akizungumza katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha hiyo iliyoandaliwa na BRELA kwa wadau wa michezo nchini, Bw. Nyaisa alisema matumizi ya picha za wanamichezo ambao wana mikataba na vilabu au taasisi husika kwa sasa limekuwa tatizo, na kwamba huwezi kutumia picha za wanamichezo kibiashara bila kuwa na makubaliano maalumu na vilabu au taasisi ambazo wanamichezo hao wanazitumikia.

Kwa upande wake Afisa Sheria kutoka Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Thadeus Almas akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza hilo Bi. Neema Msitha alisema warsha hiyo ni muhimu kwa sekta ya michezo nchini na kwamba Baraza litaendelea kushirikiana na BRELA kuhakikisha elimu wanayoipata wadau hao inakwenda kusaidia kukuza na kuendeleza sekta ya michezo na kuinua hadhi ya vilabu, mashirikisho na vyama mbalimbali vya michezo.

“Kwa sasa kuna kampuni nyingi za michezo ya kubashiri, lakini Je, sekta ya michezo inanufaika vipi? vilabu vyetu vinapata faida gani, huu ni wakati sasa wa Mashirikisho yetu kuhakikisha tunafaidika na kampuni hizo, sisi kama Baraza, tunaendelea kushirikiana kwa karibu na BRELA kuhakikisha elimu hii inawafikia mashirikisho na vyama vya michezo nchini ili kuhakikisha wachezaji wananufaika na bunifu zao, mfano hizi kampuni za michezo ya kubashiri zinapaswa kuingia makubaliano na shirikisho letu kuhakikisha vilabu vyetu vipata faida na sekta nzima inanufaika.” alisisitiza Bw. Almas

BRELA imeandaa warsha hiyo ya siku moja na kuwakutanisha wadau wa michezo nchini ikiwemo taasisi mbalimbali za michezo ikiwemo Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania COSOTA kwa lengo la kuwaongeza uelewa kuhusu masuala ya Miliki Ubunifu na kuhakikisha bunifu zinaozalishwa katika sekta ya michezo zinalindwa na kutumika kama sehemu ya kuchochea maendeleo ya Taifa.