Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
WANANCHI Mkoani Tabora wamepongeza serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Kampeni ya Huduma za Msaada wa kisheria kwa jamii kwa kuwa inasaidia kutatua kero zao.
Wametoa pongezi hizo jana baada ya kuzinduliwa kwa Kampeni hiyo katika uwanja wa Chipukizi uliopo katika halmashauri ya manispaa Tabora na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wakiwemo viongozi mbalimbali.

Wakiongea na gazeti hili baadhi ya wazee na akinamama wameeleza kufurahishwa na kampeni hiyo kwa kuwa hawatumii gharama yoyote na wanaongea ana kwa ana na Wataalamu na kutatuliwa malalamiko yao.
Mzee Medeye Chabandi mkazi wa Ipuli katika manispaa hiyo amesema kuwa kampeni hiyo ni nzuri sana kwa kuwa inasaidia wananchi wasio na uwezo kifedha kupata huduma ya msaada wa kisheria na hatimaye kupata haki zao.
‘Mimi nilidhulumiwa kiwanja, nimehangaika sana kutafuta haki yangu, kila siku nilikuwa napigwa danadana tu na wahusika, lakini leo nimeonana na watoa huduma wa msaada wa kisheria, wamenisaidia sana, nimeridhika’, amesema.

Mama Cathlyne Moshi mkazi wa Mtaa wa Kanyenye ameeleza kuwa wamepokea huduma hiyo kwa mikono miwili, kwani wanakumbana na vikwazo vingi wanapokuwa wanafuatilia haki zao na wengine hawana uwezo kiuchumi.
‘Wananchi wengi wamekuwa wakipoteza haki zao au kushindwa kuzifuatilia kwa kutokujua taratibu za kisheria au kukosa Mawakili wa kuwatetea kutokana na uwezo mdogo wa kifedha’, amesema.
Akizindua Kampeni hiyo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro, Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha amesema kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha Kampeni hiyo inawafikia wananchi wote hata walioko pembezoni.

Amebainisha kuwa kampeni hiyo ina umuhimu wa kipekee kwa kuwa itapanua wigo wa wananchi kupata haki zao za kikatiba na itawajengea uelewa wa masuala mbalimbali ya kisheria ili wasiendelee kuonewa na kudhulumiwa.
‘Kupitia kampeni hii, Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kulinda, kukuza na kutetea haki za wananchi wake ikiwemo kukomesha vitendo vyo vyote vya uvunjifu wa haki za binadamu’, ameeleza.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini amefafanua kuwa kampeni hiyo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha upatikanaji haki kwa wakati kwa wananchi wote wasio na uwezo wa kugharamia Mawakili.
Amebainisha kuwa Kampeni hiyo ya Huduma za Msaada wa Kisheria ya Mama Samia itatolewa kwa wakazi wa Halmashauri zote 8 za Mkoa huo na takribani kata 40 zitanufaika.

