RAIS  wa Kenya William Ruto ametangaza kuwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kanda ya Afrika Mashariki (EAC) utawajumuisha viongozi kutoka Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kujadili hatua za kuchukua katika kutafuta suluhu ya mgogoro unaoendelea katika eneo la mashariki mwa DRC.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda, nchi hiyo imesema ilikuwa lazima kujihami kutokana na hali hiyo. Balozi wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa, Ernest Rwamucyo, alieleza kuwa hali hiyo si ya kushangaza, akisema kuwa ni matokeo ya miaka mingi ya usimamizi mbaya wa DRC katika kushughulikia mgogoro huu.

“Hali tunayokutana nayo leo ni picha halisi ya yale yaliyotokea miaka 12 iliyopita. Ni matokeo ya usimamizi mbaya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuhusu tatizo hili. Hali hii pia inaonyesha jinsi jamii ya kimataifa ilivyoshindwa kushughulikia chanzo cha mgogoro huu, na kuruhusu wahusika kufanya kazi nje ya mamlaka yao,” alisema Rwamucyo.

Rais Eilliam Ruto amesema kuwa mkutano huu, utakaofanyika katika siku mbili zijazo, utajadili mikakati ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo na jinsi ya kuhakikisha amani inarejea katika mashariki mwa DRC. Marais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa DRC wamehakikisha kuhudhuria mkutano huo.

Mgogoro wa mashariki mwa DRC umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa eneo hilo, ukihusisha vikundi vingi vya waasi na athari kubwa kwa usalama na maendeleo ya nchi hizo.