Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wakati serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited imesema imejidhatiti kuweza kufikisha huduma ya gesi nchi nzima kwa gharama nafuu.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Meneja Mauzo wa Kampuni ya Taifa Gas, Joseph Jerome alipokuwa akizungumza na waandishi wa babari katika hafla ya futari waliyoiandaa kwa watu mbalimbali.

Amesema Taifa Gas imeweza kujidhatiti kuhakikisha inapambana na ukataji wa miti unaoendelea kwasasa, kwa kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi.

“Tunawapa watu elimu kwa njia mbalimbali juu ya matumizi ya Gas lakini pia tunashirikiana na sekta mbalimbali katika kuendeleza kampeni ya matumizi ya nishati safi ambapo juzi tumetoa mitungi elfu 10 ili kuhamasisha watu watoke kwenye matumizi ya nishati chafu na waingie kwenye matumizi ya nishati safi,” amesema.

Amefafanua, wamekuwa na kikundi kinaitwa ‘Wanawake na Samia’ ambapo wameweza kuwapa elimu ya matumizi ya gesi pamoja na kuwapa duka ambalo watakuwa wanalisimamia na kuuza ili kujipatia kipato, huku lengo ni watu waweze kupata elimu kupitia maduka hayo.

“Pia bei ambazo tumeziweka kwenye soko ni nafuu, sisi kama Taifa Gas tumejidhatiti kuweza kufikisha huduma ya gesi kote nchini lakini huduma zetu hazijaweza kuangalia zaidi tumepeleka wapi ila tumeweza kuangalia zaidi mtanzania anaenda kupata nini.

“Kwahiyo tumeangalia unafuu wa huduma zetu pale inapokwenda. Unakuta kama eneo la Kigoma bei ni 24,000 inatofautiana kidogo na Dar es Salaam kwa sh 1000 kwahiyo bei ziko vizuri mtanzania yeyote anaweza kumudu. Tuna vituo balimbali kwaajili ya urahisi na unafuu wa upatikanaji wa huduma zetu, ili kuhakikisha kila mtanzania anafikiwa na huduma ya gas. Tumekuwa bega kwa bega na serikali kuhakikisha nishati inamfikia kila mtanzania,” amesema.

Aidha amesema matumizi ya gesi ni rahisi ukilinganisha na matumizi ya mkaa ambapo ni ghali na yana madhara kwa afya ya binadamu.

“Ukiangalia mtu anayetumia mkaa na gesi kiujumla mimi ninamuona anayetumia mkaa ni Tajiri zaidi kwani anayetumia mkaa kwa mwezi atatumia120,000 kwa mtu mwenye familia ya watu watano, lakini ukiwa na Taifa Gas utatumia sh 55,000 kwa mtungi wa kilo 15,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Mambo ya Biashara, Bhoke Angellah amesema takwimu zinaonesha kuwa, takribani watu elfu 33 wanapoteza maisha kwa mwaka kutokana na matumizi ya mkaa na kuni kutokana na moshi.

“Watu hawa wanaopoteza maisha wengi wao ni wanawake sababu ndio mara nyingi wanakuwa jikoni. Kwahiyo sisi kama Taifa gas tumelitambua hilo na ndio maana tumeweka mikakati ya kutosha. Juhudi zetu nyingi tunaziweka kwa kinamama ambao wao kwa namna moja au nyingine wanafanya maamuzi kuhusu nishati ipi anaitumia akiwa jikoni

“Kwahiyo kina mama wana jukumu kuhakikisha anatumia nishati safi na kuna dhana kuwa chakula kinachopikiwa gas sio kizuri hususani wali, hii sio kweli hiyo dhana tuiondoe na waandishi wa habari tunaomba mtusaidiane kuelimisha jamii kuhusiana na hili, watu elfu 33 ni wengi kuwapoteza,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share