Taifa Stars ipo tayari kwenda AFCON

Na Tatu Saad, JAMHURI MEDIA

Baada ya kuweka kambi huko nchini Misri na kuanza mazoezi kwajili ya mchezo wa mzunguko watatu wa kundi F,kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, Kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche ameeleza namna ambavyo kikosi chake kipo tayari kwa Mchezo huo.

Amrouche amesema amefurahishwa na uwajibikaji wa mchezaji mmoja mmoja na morari ya timu kwa ujumla kuelekea katika mchezo huo licha ya kuwa na muda mfupi wa maandalizi.

Vilevile Amrouche amesema wamekuwa na maandalizi mazuri ambayo yamejikita kwenye mbinu za namna ya kucheza na kupata matokeo kwa kufanya kazi kwa ushirikiano baina ya wachezaji na benchi la ufundi.

“Tumekuwa na maandalizi mazuri ambayo yamejikita kwenye mbinu juu ya namna ya kucheza na kupata matokeo kwa kufanya kazi kwa pamoja.” Amesema Amrouche.

Kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche

Amesema hii sio mechi rahisi kwani Uganda wanatimu nzuri sana lakini atafurahi kama kikosi chake kitafanya vizuri katika michezo yote miwili kwani hawana sababu ya kusingizia wao kama timu wanatakiwa kuwapa furaha watanzania.

“Hatuna sababu ya kusingizia, hii ni timu na tunapaswa kuwapa furaha Watanzania, nitafurahi kuona tunafanya vizuri kwenye michezo yote miwili dhidi ya Uganda na sote tunafahamu (Waganda) walivyo na timu ngumu na shindani,” amesema Amrouche.

Aidha amesema yeye ni kocha mwenye mtazamo chanya hivyo anaamini kikosi chake kitapambana kupata matokeo mazuri kutokana na uwepo wa wachezaji wazuri na wenye uzoefu.

“Siku zote nimekuwa Kocha mwenye mtazamo chanya, hivyo naamini kuwa tunaweza kupambana na kupata matokeo mazuri kwa sababu tunao wachezaji wenye ubora na hata uzoefu,” amesema kocha huyo.

Mchezo wa mzunguko watatu wa kundi F wa kuwania kufuzu fainali ya Mataifa Afrika (AFCON 2023) dhidi ya Uganda ‘The Cranes’ utapigwa kesho Ijumaa ya Machi 24, katika uwanja wa Siez Canalmjini Ismailia huko Misri.