Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) wilayani Chato mkoani Geita, imetishia kuviburuza mahakamani vyama vya msingi (Amcos) vinavyodaiwa kupora hela za Chama Kikuu cha ushirika cha “Chato Co-operative Union (CCU).

Aidha imeagiza kupewa nyaraka zote za kupokea fedha na namna zilivyotumika katika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/24 na kwamba taarifa hiyo ikabidhiwe ndani ya siku 15.

Agizo hilo limetolewa na Ofisa wa TAKUKURU Wilaya ya Chato, Felix Vedastus, kwenye mkutano mkuu wa Chama cha ushirika cha CCU kilichoketi kwajili ya kupitisha makisio na ukomo wa madeni kwa mwaka 2024/25 pamoja na kuchagua bodi mpya ya chama hicho.

Wajumbe wapya wa bodi ya uendeshaji ya CCU

“Nimesikia baadhi ya Amcos zilipokea fedha kwaajili ya kununulia pamba lakini ninyi mkazifanyia matumizi mengineā€¦hili haliwezekani hata kidogo sisi Takukuru tupo karibu yenu na sasa ninaagiza vyama vyote vya msingi vinavyodaiwa fedha hizo mtuletee ofsini kwetu nyaraka zote mlizopokelea fedha na namna mlivyozitumia ndani ya siku 15 muwe mmetuwasilishia” amesema Vedastus.

Hatua hiyo imekuja baada ya Kaimu meneja wa Chama kikuu cha ushirika Chato, Berino Msigwa,kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa zipo baadhi ya Amcos wanachama wa CCU ambazo zilipokea fedha za ununuzi wa pamba lakini zikatumia kwa matumizi mengine kinyume na maelekezo ya mikataba yao.

Kadhalika amesema katika mpango mkakati wa kujiimarisha kiuchumi,chama hicho kinatarajia kutumia zaidi ya bilioni 11.5 katika ununuzi wa zao la pamba kwa msimu wa 2024/25 pamoja na kusimika mitambo ya kuchakata mafuta ya kula yatokanayo na zao hilo.

Kaimu Meneja wa Chama kikuu cha ushirika Chato(CCU) l, Berino Msigwa,akitoa ufafanuzi mbalimbali kwenye mkutano mkuu.

Kusimikwa kwa mitambo ya kuchakata mafuta ya kula inatarajiwa kuongeza uchumi wa kampuni hiyo,kuongeza ajira kwa vijana,kuondoa adha ya kupatikana kwa mafuta katika jamii pamoja na kuchangia pato la halmashauri na serikali kuu kwa ujumla.

Aidha mkutano huo umefanya uchaguzi wa wajumbe wapya wa bodi ya uendeshaji ambao watadumu kwa miaka mitatu huku msimamizi wa uchaguzi huo kutoka Tume ya maendeleo ya ushirika makao makuu,Jackson Mushumba, akimtangaza Johnson Mudandu( Kilimo kwanza) kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo na Kulwa Lukuba,akichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.

Wajumbe wengine wa bodi ni Emmanuel Ndalahwa,Mussa Method na Petro Bikira.

Mrajis Msaidizi wa ushirika mkoani Geita,Doreen Mwanri,ametumia fursa hiyo kuzitaka Amcos wananchama wa CCU kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wanapaswa kuwa wabunifu wa miradi itakayosaidia kuinua kiuchumi vyama vyao vya msingi ikiwemo kujikita kwenye ununuzi wa mazao mengine badala ya zao moja tu la pamba.

Mrajis msaidizi wa ushirika mkoa wa Geita, Doreen Mwanri,akitoa maelekezo ya serikali.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa CCU wakiendelea kusikiliza maelezo ya bodi ya usimamizi.