TAKUKURU Ruvuma yafuatilia utekelezaji miradi 19 yenye thamani ya bil. 4.5/-

Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Ruvuma (TAKUKURU), imefanikiwa kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo 19 yenye thamani ya jumla ya sh. Bilioni 4.5 ambapo mapungufu machache yalibainika ambayo yalitolewa mapendekezo ya maboresho kwa mamlaka husika .

Akitoa taarifa kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma, Janeth Haule kwa waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano uliopo kwenye ofisi hizo, amesema kuwa tayari miradi iliyokuwa imebainika kuwa na mapungufu makubwa ilishaanza kufanyiwa na hatua mbalimbali zilichukuliwa kuondoa mapungufu hayo.

Moja ya Madara yaliyojengwa kwa fedha za maendeleo mkoani Ruvuma

Kaimu Kamanda Janeth ameitaja miradi hiyo iliyofuatiliwa kuwa katika Wilaya ya Tunduru idara ya elimu ujenzi wa madarasa ,jengo la utawala pamoja na vyoo katika shule nne zote zina thamani ya sh. 911,428,792.16 na Wilaya ya Namtumbo wamefuatilia ujenzi wa madarasa, jengo la utawala vyoo katika shule vinne vyote vikiwa na thamani ya sh.849,216,795.42.

Amesema kuwa katika Wilaya ya Nyasa wamefuatilia ujenzi wa madarasa, jengo la utawala pamoja na vyoo katika shule nne vyote vikiwa na thamani ya sh. 602,500,000.00 na kwamba Wilaya ya Songea wamefuatilia ujenzi wa madarasa,jengo la utawala, vyoo pamoja na mabwalo katika shule 7 zenye thamani ya sh. 2,206,162.00.

Aidha Janeth amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma ilipokea jumla ya taarifa 38 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo mbalimbali na malalamiko yote yalifanyiwa kazi kati ya malalamiko 38 malalamiko 27 yalihusu rushwa ambapo malalamiko 11 hayakuhusu rushwa , na malalamiko 27 yalihusu rushwa na tayari katika kipindi hicho mashtaka matatu yamefikishwa mahakamani kesi zinaendelea.

Aidha amesema kuwa TAKUKURU mkoani humo itaendelea kuelimisha wananchi juu ya rushwa na madhara yake katika usimamizi wa miradi ya maendeleo lengo ni kuwawezesha wananchi kupata uelewa na kuweza kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa karibu na weledi wa hali ya juu na si vinginevyo.