DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni, amesema wanachunguza matumizi mabaya ya ofisi, ikiwamo udanganyifu na kutofuata taratibu za zabuni za ununuzi zinazodaiwa kutokea katika Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU).

Juni 16, 2022, Hamduni ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba hakuna taarifa inayofika Takukuru kisha ikaachwa kuchunguzwa.

“Uchunguzi ni mchakato, kama yeye (Katibu Mkuu wa Talgwu Taifa) anasema suala hilo linajulikana na limeripotiwa ofisini, nipe muda nifuatilie kujua limefikia hatua gani. Lakini hakuna taarifa inayokuja ofisini inapokewa katika chombo chetu cha uchunguzi halafu ikae bila kufanyiwa kazi.

“Hiyo haiwezi kutokea kwa urahisi kama anavyofikiri. Mimi naamini linafanyiwa kazi, naomba unipe muda tu nijue limefikia katika hatua gani kisha nitakujulisha,” amesema.

Kuhusu gari analotumia Katibu Mkuu wa TALGWU Taifa, Rashid Mtima, kwa ajili ya shughuli za ofisi yake lenye namba za usajili T 327 DPP kugubikwa na utata baada ya bima yake iliyokatwa kwa mara ya kwanza kuonyesha limenunuliwa kwa Sh milioni 70 badala ya Sh milioni 180, Hamduni amesema hilo ni kosa la wazi na mamlaka sahihi ya kufanya uchunguzi kwa sasa ni Jeshi la Polisi. 

“Si kila kosa linatakiwa kuchunguzwa na Takukuru, kwa mfano hilo la gari kukatiwa bima tofauti na thamani yake ni kosa la wazi kabisa chini ya Penal Code na Jeshi la Polisi ndio wanaotakiwa kuanza kulifanyia uchunguzi,” amesema. 

Juni 7, 2022, JAMHURI liliripoti habari ya utata huo wa bima ya gari hilo ambalo ni mtumba (used) huku mchakato wa ununuzi wake nao ukiwa umegubikwa na utata mwingine, kwa kuwa tangu liliponunuliwa Desemba 24, 2018 baada ya Talgwu kulipa malipo ya awamu ya kwanza (Sh milioni 40) na wakakabidhiwa Januari 2, 2019 na muuzaji akiwa ni Dar es Salaam Motors and Commission Agent Ltd, aliyepo makutano ya Mtaa wa Swahili na Barabara ya Morogoro eneo la Fire jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa waraka wa Januari 3, 2019 ambayo ni ankara ya malipo ya fedha baada ya kupatiwa huduma ya bima mseto au bima kubwa (JAMHURI lina nakala ya kivuli chake) kutoka Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwenda Talgwu inaonyesha namba za usajili wa gari hilo ambazo ni T 327 DPP, aina yake ni Toyota na thamani yake ni Sh milioni 70.

Kutokana na utata huo wa bima, Juni 3, 2022 JAMHURI liliwasiliana na ofisa mmoja wa ZIC kwa njia ya simu (hakutaka jina lake liandikwe gazetini) akasema Talgwu ndio waliofanya kosa kwa kutoa taarifa za uongo za thamani halisi ya gari hilo.

Katika hatua nyingine, Juni 3, 2022, JAMHURI liliwasiliana kwa njia ya simu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa ZIC, Arafat A. Haji, akaliambia JAMHURI liende ofisini kwao Tawi la Lumumba, Dar es Salaam kupatiwa ufafanuzi zaidi wa taarifa ya utata huo hadi wakalikatia bima.

“Wateja wengine wanatoa thamani kubwa ya magari yao ili yanapopata ajali alipwe fedha nyingi na wengine wanatoa thamani ndogo ili tozo ya bima watoe ndogo,” amesema Arafat.

 Juni 3, 2022 akizungumza kwa njia ya simu na JAMHURI, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Oyuke Phostine, amesema ni kosa kisheria kwa mteja kutoa taarifa za uongo kuhusu thamani ya gari na ikigundulika adhabu yake ni kufutiwa bima yake kwa kuwa si halali.

Utata ununuzi wa magari 

14 ya makatibu wa mikoa

Pia chanzo hicho kimesema mwaka 2019, Talgwu, imefanya ununuzi wa magari 14 ambayo ni mitumba kwa makatibu wake wa mikoa yenye thamani ya Sh milioni 540 kwa pamoja bila kufuata taratibu na kanuni zinazosema zabuni inayozidi Sh milioni 80 itangazwe kwa umma.

Licha ya kuwa ni mitumba lakini chanzo hicho kimesema ofisi ya Mtima imetoa taarifa katika kikao namba 27 cha Baraza Kuu la Talgwu Taifa kilichofanyika Januari 15-16, 2022 katika Hoteli ya Royal Village, Dodoma kwamba imeratibu mchakato wa ununuzi wa magari mapya.     

Vilevile kimesema ununuzi wa magari hayo aina ya Toyota Land Cruiser Prado yaliyotengenezwa kati ya mwaka 1996 na 1999 uliidhinishwa na Mtima akiwa ndiye ofisa masuhuli wa Talgwu na kupelekwa mikoani.

Kimetaja namba za usajili za magari hayo katika mabano na mkoa yalikokwenda kuwa ni Dar es Salaam (T 321 DVE), Morogoro (T 432 DVB), Mtwara (T 318 DVE), Dodoma (T 338 DVE), Katavi (T 397 DVB), Rukwa (T 379 DUS), Mara (T 584 DUN), Tabora (T 126 DUK), Shinyanga (T 583 DUN), Pwani (T 684 DVD), Lindi (T 395 DVB) na makao makuu (T 582 DUN) huku yakiwa ni chakavu kwa sababu yametengenezwa na kutumika zaidi ya miaka 25 iliyopita na yamenunuliwa kati ya Sh milioni 38 hadi Sh milioni 40, na yamekwisha kutembea zaidi ya kilomita 260,000 hadi 300,000.

Mtima ajibu

Mei 14, 2022, JAMHURI lilizungumza na Mtima kwa njia ya simu yake ya mkononi na kumtaka mwandishi wa habari hii kwenda ofisini kwake kwa ajili ya kupata majibu yote.

“Nitakupa usahihi wa hizo kadi, mbona hizo kadi walifuatilia mwaka jana? Gari limenunuliwa tangu mwaka 2019 hadi leo hayo mambo ya kadi yanatoka wapi? Ionekane lina kadi mbili?” amehoji.

Mei 16, 2022, JAMHURI lilifika ofisi za Talgwu na kuzungumza na Mtima na amesema mwaka 2020 aliingia katika kinyang’anyiro cha ubunge na akasumbuliwa na maofisa wa Takukuru lakini akawaambia siku watakapomchukua kwa sababu wametumwa kumwaribia, kumdhuru na kumpeleka Mahakama ya Kisutu jamii yote itawashangaa.

Amesema Takukuru imeundwa ili kurekebisha jamii na kuna siku itaonyesha kwamba inawaonea watu.

Kuhusu gari analolitumia kuwa na kadi mbili na licha ya kumhakikishia mwandishi wa habari hii kwamba akienda ofisini kwake atamuonyesha, lakini hakufanya hivyo kisha naye akazihoji. 

“Sasa kadi mbili kivipi? Kwamba kuna kadi ya kwangu halafu kuna kadi ya Talgwu?” amehoji.

Amekiri kwamba gari hilo wamelinunua kwa Sh milioni 180 baada ya kwanza kutenga Sh milioni 100 ambazo  hazikutosha kutokana na bei za sokoni, kisha wakaongeza Sh milioni 80.

“Ninachojua kadi ni moja tu na wamechukua Takukuru. Kwa hiyo kama kuna kadi mbili sikumbuki kabisa na kama ni kweli, basi hata TRA nao wana vitendo vya rushwa,” amesema.

Kuhusu ununuzi wa magari 14 amesema ameanza kazi Talgwu Septemba, 2016 kisha akayapokea manne yaliyonunuliwa kwa Sh milioni 45 kila moja, kisha akanunua mengine ya aina hiyo kwa Sh milioni 40 lakini yanapigiwa kelele za rushwa.

By Jamhuri