Na Agnes Njaala, JamhuriMedia, Rukwa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuanza rasmi kwa zoezi la maboresho ya mfumo wa LUKU ambapo sasa ni zamu ya mikoa ya Kanda ya Kusini na Nyanda za juu Kusini Magharibi.
Akitangaza kuanza rasmi kwa zoezi hilo kupitia ziara ya utoaji wa elimu kwa Wateja kupitia vituo mbalimbali vya redio katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Mbeya , Songwe, Rukwa na Iringa hapo jana , Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TANESCO Bi. Irene Gowelle amesema ,tayari zoezi hilo lilishaanza katika Mikoa ya kanda ya Ziwa na kanda ya Magharibi, na kwamba kuanzia tarehe 24/06/2024 limeanza rasmi katika mikoa ya kanda ya Kusini na Kanda ya Nyanda za juu Kusini Magharibi.
Bi. Gowelle amesema malengo ya Shirika kufanya maboresho hayo ni kuendana na mabadiliko ya kimfumo ya viwango vya mita za LUKU vya kimataifa , vilevile kuongeza ufanisi na usalama wa mita za LUKU nchini.
Akielezea namna ya kufanya maboresho hayo amesema ” Kuanzia tarehe tajwa kwenye mikoa husika iliyotangaziwa kuanza maboresho hayo jana, Mteja atakapofanya manunuzi ya umeme kupitia risiti yake ya malipo au ujumbe wa simu atapokea makundi matatu yenye jumla ya tarakimu sitini (60) kila kundi likiwa na tarakimu ishirini (20) ambapo makundi mawili ya mwanzo yatakuwa ni kwa ajili ya maboresho (Key change tokens) na kundi moja la mwisho litakuwa ni umeme ambao utakuwa umenunuliwa na mteja”.
Mteja ataingiza makundi yote ya tarakimu kwa kufuata mpangilio kama utakavyokuwa unasomeka kwenye risiti ya malipo na kwa kubonyeza alama ya reli # au mshale wa kukubali kila baada ya kuingiza kundi moja na baada ya hapo mteja atakuwa amekamilisha kufanya maboresho na kuingiza umeme wake alionunua.
Katika hatua nyingine amebainisha kuwa, zipo changamoto ambazo wamezipata katika mikoa iliyoanza zoezi la maboresho ikiwemo uelewa wa namna ya kuingiza token za maboresho na baadhi ya mita kubainika kushindwa kupokea mabadiliko hayo.
Ameshauri iwapo mteja yoyote atapata changamoto hiyo apige simu kwa namba za huduma kwa wateja katika mikoa husika ambapo wataalamu wa TANESCO watakapofika na kubaini mita ina changamoto basi Shirika litawajibika kumbadilishia mteja huyo mita bure bila gharama yoyote.
Vilevile Bi. Gowelle alisisitiza kuwa, ni muhimu Wateja wote kufahamu kuwa iwapo walifanya manunuzi ya umeme nyuma kabla ya zoezi hili kuanza, watapaswa kuingiza umeme huo kwenye mita zao kabla ya kufanya maboresho hayo kwani kutokufanya hivyo kutafanya umeme wao kupotea kwani mara baada ya mabadiliko tajwa kufanyika, umeme wa zamani hautatambulika tena kuweza kuingia kwenye mita na hivyo utahesabika kuwa umepotea.
Zoezi la maboresho ya mfumo wa LUKU ni zoezi la bure halina gharama yoyote kwa Mteja na ukomo wa zoezi hili kote nchini ni Novemba 24, 2024 na TANESCO inaendelea na maboresho haya katika mikoa yote nchini kwa awamu hivyo, wateja wote ambao bado hawajafikiwa na zoezi hili wanaombwa kuendelea kuwa watulivu na kuendelea kupokea elimu inayoendelea kutolewa ili zoezi litakapofika kwenye mikoa yao iwe rahisi kwao kufanya maboresho hayo.