Tanzania na Algeria kuanza ushirikiano katika sekta ya afya, hususan katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya, uhamishaji wa teknolojia na uwekezaji, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa nchi hizo na Afrika kwa ujumla katika kujitegemea kwa bidhaa muhimu za afya.
Hayo yamesemwa leo, Oktoba 5, 2026, jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, alipokutana na ujumbe kutoka Wizara ya Viwanda vya Dawa ya Algeria pamoja na kampuni ya Les Laboratoires FRATER-RAZES, unaofanya ziara nchini Tanzania kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya.
Dkt. Magembe amesema Tanzania inaweka mkazo katika kuendeleza uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya nchini, akieleza kuwa utekelezaji wa azma hiyo unahitaji ushirikiano na nchi zenye uzoefu, pamoja na uhamishaji wa teknolojia na uwekezaji.
“Algeria imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika, hii ni fursa kwa Tanzania kujifunza na kushirikiana na nchi hiyo ili kuongeza uwezo wa uzalishaji katika nchi zote mbili” , amesema Dkt Grace
Aidha, Dkt. Magembe amesema Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya, huku ikiendelea kuimarisha taasisi muhimu zikiwemo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na Bohari ya Dawa (MSD), zenye jukumu katika udhibiti, ununuzi na usambazaji wa bidhaa za afya.
Amesema ushirikiano huo unapaswa kwenda sambamba na kukuza biashara na uwekezaji katika sekta ya bidhaa za afya, akisisitiza kuwa uzoefu wa janga la COVID-19 umeonesha umuhimu wa nchi za Afrika kujenga uwezo wa ndani wa kuzalisha bidhaa muhimu za afya ili kupunguza utegemezi na kuwa tayari kukabiliana na majanga yajayo.




