Tanzania kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Serikali ya Cuba kupitia Taasisi ya INDER ya nchini humo zimekubaliana kushirikiana katika eneo la kuendeleza mchezo wa ngumi, ambapo mabondia kutoka hapa nchini watapata fursa ya kuweka Kambi Cuba pia walimu wa ngumi na Mabondia kutoka Cuba watapata fursa ya kuja Tanzania kufundisha na kubadilishana ujuzi.

Makubaliano hayo yamefikiwa Agosti 2, 2023 wakati Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Hamis Mwinjuma alipofanya mazungumzo na Bw. Raul Fornes Valenciano ambaye ni Makamu wa Rais wa kwanza wa Taasisi hiyo ya Kitaifa ya Michezo, Elimu na Burudani ambacho ni chombo kinachohusika na ukuzaji wa michezo, elimu ya viungo na burudani nchini Cuba.

Taasisi hiyo tayari ina mashirikiano na baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Algeria ambapo hubadilishana uzoefu kwenye eneo la mchezo wa ngumi.

Naibu Waziri Mhe. Mwinjuma yupo nchini Cuba kwa ajili ya kuhudhuria maonesho ya kimataifa ya michezo ya Havana.

By Jamhuri