Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilifanya kazi kubwa ya kutuunganisha Watanzania ambao tunaishi kama ndugu bila chembe yoyote ya ubaguzi.

Maisha yetu ya kupendana, kuthaminiana na kuheshimiana bila kuangalia tofauti za makabila au uwezo wa kiuchumi alionao mtu ndiyo mazao ya amani na utulivu tulionao hadi leo.

Kwa utaratibu wa maisha yetu haya, imekuwa rahisi hata kuheshimiana, kuthaminiana na kujiona kama ndugu kwa wale wanaokutana katika mataifa ya kigeni. Hiyo imekuwa tofauti sana na raia wa nchi zingine.

Utamaduni huu sasa umeanza kupotea kutokana na matukio ya hovyo yanayojitokeza kwa kasi sana kipindi hiki, yanayofanywa na watu wa hovyo (watu wasiojulikana) kuwateka watu bila sababu za msingi.

Maharamia hawa hawakuvuma awamu zilizopita ndiyo maana kila Mtanzania amekuwa na maswali yanayokosa majibu. Je, wametumwa na nani kuvuruga amani ya Watanzania? Wananufaika namna gani na vitendo hivi? Wanamfurahisha nani?

Kwa vitendo hivyo vya uharamia na kukosa majibu ya maswali hayo, Watanzania sasa wanaishi kwa hofu kwamba huenda wakakutana na watu hao wa hovyo watakaowateka.

Hakuna tajiri wala maskini, mzawa au mgeni, mwekezaji wa ndani au wa nje asiyekuwa na hofu kutokana na matukio haya ya uovu yanayofanyika ndani ya nchi yetu ambayo ni kisiwa cha amani.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, hivi karibuni amesema jumla ya watu 75 wametekwa katika kipindi cha miaka mitatu.

Lugola alitoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku tatu tangu alipotekwa mfanyabiashara bilionea Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’, ambaye alipatikana baada ya siku tisa.

Amesema licha ya juhudi za polisi nchini, mwaka 2016 kulikuwa na matukio ya watu tisa kutekwa na kati yao watano walipatikana wakiwa hai kwa ushirikiano na wananchi.

Lugola amesema watu wanne hawakupatikana katika kipindi hicho na watuhumiwa sita walikamatwa huku watano wakifikishwa mahakamani na mmoja aliuawa na wananchi.

Amesema mwaka 2017, watu 27 walitekwa na polisi walifanikiwa kuwapata 22 wakiwa hai na wawili wakiwa wamekufa, huku watatu hawakupatikana.

Januari hadi Oktoba 11, mwaka huu watu 21 walitekwa na kati yao 17 walipatikana wakiwa hai na wanne hawakupatikana hadi sasa ambapo watuhumiwa 10 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Akielezea kuhusu watoto, amesema tangu mwaka 2016 jumla ya watoto 18 kati yao wa kiume sita na wa kike 12 walipotea.

Hata hivyo pamoja na taarifa hiyo ya Waziri Lugola na jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi, wananchi kuendelea kuishi kwa hofu ndani ya nchi yao si jambo jema.

Serikali inapaswa kuhakikisha hali ya usalama kwa wananchi kwa kufunga kamera katika maeneo yote ya miji kwa kuiga utaratibu unaotumiwa na baadhi ya nchi.

Mfano nchini Australia si rahisi watu kufanya uhalifu wowote na wasikamatwe baada ya muda mfupi, kwa sababu maeneo yote ya miji yamefungwa kamera za usalama, hivyo kwa nchi yetu kufunga kamera hizo kutasaidia kupunguza matukio ya uhalifu.

Pia itakuwa ni mbinu nyingine ya kuwavutia wawekezaji na watalii kuja kwa wingi nchini na kuwahakikishia usalama wao na mali zao na kuwaweka wazi watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

Watanzania tuilinde amani ya nchi yetu kwa nguvu zetu zote bila kukubali kuvurugwa ama kutiwa hofu na wahalifu hawa ambao wana lengo la kutugawa na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu.

By Jamhuri