TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Afrika zitakazonufaika na fedha za Mfuko wa Kukuza Uwekezaji barani Afrika kutoka Serikali ya Japan zitakazotolewa kuanzia Machi, 2023.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa timu ya Afrika ya KEIZAI DOYUKAI (Japan Association of Corporate Executives), Bw. Mutsuo Iwai wakati akizungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ofisini kwao Marunouchi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo, Japan.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akioneshwa kaburi la pamoja la askari wa Jeshi la Zimamoto, waliyopoteza maisha kwenye harakati za uokoaji  na Rais wa taasisi ya Zimamoto ya Japan, Kamishna Akimoto Toshifumi ofisini kwao Higashi-Shimbashi, jijini Tokyo, Japan.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Ifikapo Desemba mwaka huu, tutazindua kampuni ya kusimamia mfuko huu wa uwekezaji wenye manufaa barani Afrika na utekelezaji utaanza Machi, 2023. Tunataraji ifikapo Machi, 2024 tutakuwa tumetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 100 kwa kampuni za vijana wanaochipukia ili kuwajengea ubia, kujifunza teknolojia mpya na kubadilishana ujuzi,” amesema.

Amesema fedha hizo za uwekezaji kwenye mitaji (start-ups) zimelenga kukuza biashara ambazo zitatatua changamoto za kijamii zikiwemo sekta za afya, kilimo, nishati na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Rais wa taasisi ya Zimamoto ya Japan, Kamishna Akimoto Toshifumi (kulia) baada ya kikao kilichofanyika ofisini kwao Higashi-Shimbashi, jijini Tokyo, Japan. Katikati ni Naibu Mkurugenzi wa Masuala ya Kimataifa Fukushi Hiroshi.

Utolewaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida aliyoitoa Agosti 27, 2022 wakati akitoa hotuba kwenye Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) uliofanyika jijini Tunis, nchini Tunisia.

Waziri Mkuu Kishida alisema Japan imelenga kukuza uwekezaji ambapo safari hii wamelenga kuwainua vijana wanaoanzisha makampuni kwani hatua hiyo itawapa fursa vijana wa Afrika na wa Japan kufanya kazi kwa karibu.

KEIZAI DOYUKAI ni taasisi binafsi iliyoanzishwa Aprili 30, 1946 yenye wanachama wapatao 1,500 ambao ni watendaji wakuu na wamiliki wa makampuni makubwa ya Japan wanaojihusisha na utoaji suluhisho kwa masuala ya kisera yanayohusu maendeleo ya nchi yao na dunia kwa ujumla.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa taasisi ya Zimamoto ya Japan, Kamishna Akimoto Toshifumi, kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwao Higashi-Shimbashi, jijini Tokyo, Japan. 

Waziri Mkuu pia alikutana na wawakilishi wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Japan (KEIDANREN) ofisini kwao Otemachi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo, ambako Mwenyekiti wa Kamati ya nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Hajime Kawamura alimweleza jinsi shirikisho lao linavyojihusisha na miradi ya maji, barabara, nishati, mawasiliano utengezaji wa kemikali na ununuzi wa mazao.

Wawakilishi wa kamati hiyo wanaotoka makampuni ya Sumitomo, Marubeni, Toshiba, Komatsu na Mitsubishi walimweleza Waziri Mkuu nia yao ya kuwekeza kwenye miradi ya nishati ikiwemo uzalishaji wa umeme kwa kutumia jotoardhi, usambazaji wa umeme, usambazaji wa gesi (LPG), huduma za mawasiliano na TEHAMA.

KEIDANREN (Japan Business Federation) jumuiya ya kiuchumi iliyoanzishwa Agosti 16, 1946 yenye wanachama 1,494 ambao ni wawakilishi wa makampuni ya Kijapani, ina vyama 108 vya wenye viwanda na taasisi 47 za kiuchumi kutoka mikoa yote.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu aliwaeleza wafanyabiashara wa makundi yote mawili kwamba Serikali ya awamu ya sita iko tayari kufanya kazi na wawekezaji na ndiyo maana iliamua kuboresha miundombinu ili kurahisha upatikanaji wa huduma muhimu.

“Utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, utulivu na amani vilivyopo nchini, hali nzuri ya hewa, ujenzi wa bandari, reli na barabara, umeme na maji unawahakikishia wawekezaji uhakika wa mitaji pindi mnapoamua kuwekeza nchini Tanzania,” alisema.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Kamati ya nchi zilizo Kusini mwa Sahara, Bw. Hajime Kawamura, ilipowasili ofisini kwao Otemachi, jijini Tokyo, Japan. 

Waziri Mkuu aliwahamasisha waje nchini kuwekeza kwenye sekta ya utalii ikiwemo ujenzi wa hoteli za nyota tano na kuanzisha michezo ya majini kwenye fukwe za bahari Zanzibar na Bara. “Pia angalieni uwezekano wa kuwekeza kwenye kilimo cha mashamba makubwa na ujenzi wa viwanda. Lengo la Serikali hii ni kuendelea kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo viwanda,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alikutana na Rais wa taasisi ya Zimamoto ya Japan, Kamishna Akimoto Toshifumi na kujadiliana uwezekano wa taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa askari wa jeshi la uokoaji na zimamoto nchini.

Mikutano hiyo yote ilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Wawakilishi wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Japan (KEIDANREN) ofisini kwao Otemachi, jijini Tokyo, Japan.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiagana na Mwenyekiti wa timu ya Afrika ya KEIZAI DOYUKAI, Bw. Mutsuo Iwai, baada ya kikao kilichofanyika Marunouchi, jijini Tokyo, Japan.
Please follow and like us:
Pin Share