Na Wilson Malima Dar es Salaam.

Shirika la ndege Tanzania (ATCL) linatarajia kupokea ndege ya abiria ya masafa ya kati aina ya B737-9MAX ambayo uundaji wake umekamilika itakayowasiri kesho Oktoba 03, 2023.

Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 181 katika madaraja mawili ambapo daraja la kawaida “economyclass” itabeba abiria 165 na darajala biashara (business class) abiria 16, pia ina uwezo wa kubeba mzigo wa tani 6 na kuruka wastani wa masaa 8 bila kutua.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa leo Oktoba 02, 2023 amesema sasa ATCL itakuwa na ndege 13 zilizonunuliwa na serikali kuanzia 2016 na kuwa na ndege 14 zinazosimamiwa na shirika hilo

“Kuwasili kwa ndege hiyo kutaifanya ATCL kuwa na ndege 13 mpya zilizonunuliwa kutoka na utekelezaji wa mpango mkakati wa Serikali ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2016 na hivyo kuwa na ndege 14 zinazosimamiwa na ATCL katikauimarishaji wa wigo wa mtandao wa safari zake ndege kwa soko la ndani, kikanda na kimataifa.” Amesema Prof. Mbarawa.

Amesema, ujio wa ndege hiyo ya kisasa ya masafa ya kati aina ya B737-9 MAX kutaiwezesha ATCL kuongeza vituo vya Pemba,Tanga,Mafia,Nachingwea, na Musoma katika mtandao wa safari za ndani. Pia itaongeza miruko ya safari za usiku kwa viwanja vya ndege ambavyo vina taa pamoja na kuanzisha safari za usiku katika viwanja vya ndege vya Dodoma na Songea ambavyo miradi ya ufungaji wa taa za kuongozea taa imekamilika.

Sambamba na hilo Prof. Mbarawa amesema katika kuiimarisha ATCL serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha ndege zinazonunuliwa zinakuwa na wataalamu wa ndani wa kuzihudumia ili kupunguza gharama za kutumia wataalam wa nje hususan Marubani na Wahandisi ndege ikiwa ni pamoja na kukijengea uwezo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kujenga miundombinu wezeshi, mitambo, vifaa pamoja na ununuzi wa ndege za mafunzo .

“Ndege hizo zitatumiwa na NIT kutoa mafunzo ya Urubani kwa darajala awali (PPL)ambayo yatachukua miezi 6 kwa ada ya TZS 21,000,000/= na daraja la biashara (CPL) ambayo yatachukua miezi 12 kwa ada ya TZS 53,800,000/=) na kufanya jumla ya ada kwa mafunzo yote kuwa TZS 74,800,000/= ambayo ni ndogo ukilinganishwa na gharama za kusoma mafunzo haya nje ya nchi ambayo kwa wastani hugharimu TZS 300,000,000/=. Kwa kuwa ndege moja (1) inaweza kutumika kufundishia wastani wa wanafunzi watano (5), Chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 10 kwa mkupuo mmoja.” Amesema

Itakumbukwa kuwa mwaka 2016, Serikali ilichukua hatua za kuifufua Kampuni yaNdege Tanzania (ATCL) kwa kuanza kuinunulia ndege na kufanya mabadiliko ya Menejimentina Bodi ya Wakurugenzi.

Hadi Septemba, 2023ATCL imeshapokea ndege 12 mpya ambazo zimenunuliwa na Serikali. Ndege hizo ni:ndege mbili kubwa aina ya B787-8 Dreamliner ambazo zinauwezo wa kubeba abiria 262 kila moja; ndege nne za masafa ya kati aina ya Airbus A220-300 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja; ndege tano za masafa mafupi aina ya D8 Q400 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila mojana ndege kubwa ya mizigo aina ya B767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54.

By Jamhuri