Na Shamimu Nyaki, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kuwasilisha ombi la kuweka matangazo kwa lugha ya Kiswahili katika Mashindano ya Kombe la Mataifa Barani Afrika AFCON yatakayochezwa mapema mwaka 2024.

Ndumbaro amesema hayo Oktoba 16, 2023 alipofanya ziara Ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), ambapo amepongeza juhudi za Baraza hilo katika kubidhaisha lugha hiyo Kimataifa pamoja na kuzalisha wakalimani na Watafsri mbalimbali.

Amesema, Tanzania ikishirikiana na Kenya na Uganda imefanikiwa kupata uwenyeji wa mashindano hayo mwaka 2027 ambayo ni fursa ya kutangaza lugha  ya Kiswahili  katika mashindano hayo.

“Tunataka Kiswahili kitengeneze fursa nyingi, mwaka wa fedha wa 2024/25 tutatenga fedha kwa ajili ya kuuza lugha hii ambayo kwa sasa imeajiri Watanzania 103 Duniani, pamoja na kushirikiana na Sekta Binafsi katika kubidhaisha lugha yetu adhimu ya Kiswahili” amesisitiza Mhe. Ndumbaro.

Awali Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Consolatha  Mushi ameeleza kuwa, katika Mkakati wa miaka kumi wa Kubidhaisha Kiswahili wa 2022 Р2032,  tayari wamefungua vituo 32 ambavyo 10 vipo katika Balozi za Tanzania na tayari limepokea maombi ya kuanzisha vituo vya kujifunza lugha hiyo kwa nchi za Ufaransa na Uturuki.

Consolatha amesema nchini Urusi kuna Vyuo Vikuu vitano ambavyo lugha hiyo inatumika kikiwemo Chuo Kikuu cha Moscow pia inatumika katika shughuli za Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (SADC)