Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Okyoba 5, 2023 ametangaza rasmi kuwepo kwa siku maalum ya kuthīamini mchango wa kazi ya Mwalimu katika Mkoa huo.
RC Chalamila amesema hayo wakati akihutubia mamia ya walimu waliokusanyika katika hafla hiyo viwanja vya Mnazimmoja Ilala jijini Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani ambayo yamefanyika katika ngazi ya mkoa.”
Walimu watakua na siku maalum ambayo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa wale wanaofanya vizuri pia kutakuwa na usiku wa mwalimu siku hiyo atakua na uwezo wa kuongea na viongozi akiwa huru hata kama ana Changamoto aziseme, wakati mwingine imekuwa ngumu kumfikia kiongozi hiyo sasa ni fursa” amesema RC Chalamila.
Albert Chalamila alipata wasaa wa kusikiliza mafanikio na Changamoto za kada hiyo ikiwemo maombi ya kupatiwa Teaching allowance, malipo ya likizo, Kikokotoo wakati wa kusitaafu, uhaba wa nyumba za walimu, ambapo amesema yale yote yaliyoko ndani ya uwezo wake yatafanyiwa kazi kwa wakati.
Aidha RC Chalamila amewataka walimu kuchapa kazi kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia anawapenda walimu na dhamira yake inajidhihirisha wazi kutokana na uwekezaji mkubwa anaoufanya katika sekta elimu, kama uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya elimu, kupandisha mishahara, ajira za walimu, elimu bila malipo, mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu na sasa ameshafungua dirisha kwa wanafunzi wa astashahada nao wanayo fursa za mikopo.
Kwa upande Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Dar es Salaam Justine Runyoro amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuja kushiriki nao katika maadhimisho hayo kwa namna ya kipekee wamefarijika sana, ni imani yao kuwa Sekta ya Elimu katika Mkoa huu inakwenda kuboreka zaidi.
Mwisho Albert Chalamila ametoa wito kwa walimu kuepuka mikopo umiza ambayo ina riba kubwa na kuwataka kuratibu semina elekezi ya ujasiriamali kwa walimu ili kupata uelewa wa kujiongezea kipato hatimaye kujikwamua na wimbi la umasikini.