Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Aliyekuwa Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Gerson Msigwa amekabidhi rasmi kijiti kwa mrithi wake Mobhare Matinyi huku akiahidi kuteleleza kwa vitendo majukumu yake ya sasa na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kwa kipindi chote alichohudumu kwenye Idara hiyo.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu, kufanya mabadiliko ya ngazi mbalimbali za uongozi huku Msigwa akipangwa akipewa nafasi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo leo Oktoba 5,2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-Maelezo amesema kuwa mbali na kuondoka kwenye nafasi hiyo ataendelea kuisemea Serikali pamoja na vyombo vya habari kila anapopata nafasi kwani hiyo ndo taaluma yake.

“Mabadiliko yanapokuja ni pumzi mpya na sio vita, nafurahi kuwepo kwenye nafasi yangu ya sasa lakini pia sitaacha kuwasemea waandishi wa habari niseme wazi napenda mitandao ya kijamii hasa pale ninapokuwa napewa vijembe mitandaoni huwa inanifunza , “amesema.

Kuhusu hali ya uchumi wa vyombo vya habari nchini, Msigwa meeleza kusikitishwa kwake na hali mbaya ya kiuchumi kwa waandishi wa habari na kueleza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya waandishi hao hawana ajira za kudumu jambo linalokatisha tamaa.

” Wakati nipo kwenye idara hii kipaumbele changu kilikuwa ni kushughulikia uchumi wa vyombo vya habari, nasikitika sana naondoka nikiwa sijakamilisha hili nina imani mwenzangu ataanzia pale nilipoishia,”ameeleza

Msigwa pia ameeleza mafanikio ya idara hiyo tangu aliposhika nafasi hiyo kuwa ni pamoja na kuanzisha machapisho ya kazi iendelee,nchi yetu miaka 60 ya Uhuru yote yakiwa yanasanifiwa na Idara ya Habari ,ikiwa ni pamoja na studio ya kutengeneza vipindi vya mkakati na gari la kurushia matangazo ya nje, kurasa za kimtandao kuhabarisha umma.

“Nitapambana kwa nguvu zangu zote kuhakikisha nafikia matarajio ya Rais Samia matarajio ya kuifanya wizara kuwa ajira na kutengeneza fedha kiuchumi naamini hii itasaidia kutimiza matarajio ya watanzania,mnenipa ushirikiano mzuri najivunia, naomba ushirikiano huo mmpatie kaka yangu kwani ni nguzo muhimu kwenye tasnia, “ameeleza na kuongeza;

Kati ya vitu najivunia katika Idara hii watu wote ni rafiki zangu, mafanikio mengi nimeyapata kutoka na ushirikiano wa wafanyakazi wa Idara hii,kazi ya Serikali ni kambi popote, tunajenga nchi moja na tunafanya kitu kimoja, ” amesisitiza.

Kwa upande wake Mobhare Matinyi ambaye amepewa ridhaa ya nafasi hiyo ya kuwa Msemaji wa serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo ametumia nafasi hiyo kuwaelekeza Waandishi kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia misingi ya maadili na kuichukulia habari kwa unyeti wa kipekee ili kuondoa sintofahamu kwenye jamii

“Huu wadhifa ni nyeti naahidi kuifanya kazi kwa kushirikiana na watu wote ili watanzania wapewe taarifa sahihi nashukuru Msigwa anaiacha Idara hii ikiwa na umahiri,naahidi kuendeleza yaliyobaki na kutimiza matarajio ya Serikali yetu na wananchi kwa ujumla, ” Amesema.