IMEELEZWA kuwa ugonjwa wa Kifua Kikuu ni Janga la Kitaifa na la Kidunia ambapo ni moja kati ya magonjwa yaliyokuwepo duniani kwa muda mrefu na umeshachukua maisha ya mamilioni ya watu Duniani kote.

Hayo yamesemwa jana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma unaoendelea jijini Mwanza.

Elikana amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye kiwango kikubwa cha ugonjwa wa Kifua Kikuu ikikadiriwa kuwa na wagonjwa 132,000 sawa na wagonjwa 208 katika watu 100,000. Aidha, kwa mwaka wa 2021, wagonjwa 87,415 wa Kifua Kikuu waligunduliwa na kuweka kwenye matibabu, ikiwa ni sawa na asilimia 65 ya makadirio ya WHO.

Kwa upande wa ugonjwa wa Ukoma Bw. Elikana amesema Idadi ya wagonjwa wapya wa Ukoma wanaogunduliwa nchini inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka katika miongo miwili iliyopita ambapo Dunia iliongeza kasi ya kupambana na ugonjwa huu.

“Nchi yetu imeweza kuwagundua na kuwatibu wagonjwa wapya wa Ukoma zaidi ya 121,000 na kwa mwaka 2020 walikuwepo wagonjwa wapya 1,208 tu, idadi ya watoto waliogundulika kuugua Ukoma ilifikia 41 na hivyo kuonesha wazi ya kuwa mnyororo wa maambukizi bado upo na bado tuna jukumu kubwa la kufanya kukomesha kuenea kwa ugonjwa huu nchini” amesema Elikana.

Aidha, katibu Tawala huyo amesema Jitihada za Serikali katika kutokomeza magonjwa haya nchini zinahitaji nguvu ya pamoja ya wadau wote ambapo Serikali kwa kushirikiana na wadau wameweza Kupunguza idadi ya maambukizi ya Kifua, kupunguza vifo kutoka 55,000 mwaka 2015 kufikia vifo 25,800 mwaka 2021, Kufikia hatua ya awali ya kiwango cha kimataifa cha utokomezaji wa Ukoma tangu mwaka 2006 na Kuanzisha huduma za Mkoba za Kifua Kikuu.

Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim amesema Serikali imejiwekea lengo la kutokomeza Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030 sambamba na malengo endelevu ya maendeleo.

“Ili kufikia malengo haya tunahitaji ushirikishwaji mkubwa wa jamii, wadau na sekta zote nchini katika kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu” amesema Dkt. Catherine.

By Jamhuri