Na John Mapepele, Geneva, Uswisi

Tanzania imethibitisha tena dhamira yake ya kuimarisha huduma za kinga, uchunguzi, tiba na uangalizi wa saratani kufuatia kutolewa kwa Ripoti ya Uhakiki wa Misheni ya imPACT 2025, huku Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, akiahidi kuimarisha ushirikiano na washirika wa kimataifa wakati wa kikao cha pande mbili kilichofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 79 wa Shirika la Afya Duniani (WHA) mjini Geneva.

Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Mchengerwa alisema Serikali ya Tanzania inathamini ushirikiano wake wa muda mrefu na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), hasa katika kupanua huduma za saratani na kuimarisha mfumo wa afya kupitia matumizi salama na ya amani ya teknolojia ya nyuklia.

“Hii ni mara ya pili mwaka huu kukutana na viongozi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki,” alisema Mchengerwa, akibainisha kuwa mazungumzo yaliyofanyika mwezi Februari yalijikita katika ushirikiano wa kimkakati kwenye huduma za saratani, ikiwemo uwezekano wa kuanzishwa kwa kitengo cha kikanda cha mafunzo na huduma za pamoja.

Waziri huyo alieleza kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na IAEA kupitia zaidi ya miradi 12 ya afya inayolenga kuboresha huduma jumuishi za saratani. Miradi hiyo inahusisha kuimarisha mifumo ya taarifa za saratani, kampeni za kinga na uhamasishaji, kujenga uwezo wa wataalamu pamoja na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya uchunguzi na matibabu.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, Tanzania pia imenufaika na Mpango wa Ushirikiano wa Kiufundi wa IAEA, ikiwemo kushiriki katika tathmini ya imPACT pamoja na mpango wa Rays of Hope, ambayo inalenga kuimarisha huduma za kudhibiti saratani barani Afrika.

Misheni ya Uhakiki wa imPACT 2025 ilifanya tathmini ya uwezo wa Tanzania katika huduma za saratani katika mnyororo mzima wa huduma, na kuwa tathmini ya pili kubwa kufanyika nchini ndani ya karibu muongo mmoja. Ripoti hiyo inatoa tathmini huru inayotegemea ushahidi kuhusu maendeleo yaliyopatikana pamoja na kubainisha maeneo ya kipaumbele yanayohitaji hatua za haraka.

Mchengerwa alisema muda wa kutolewa kwa ripoti hiyo ni muhimu kwa kuwa unaendana na mapitio ya Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya wa Tanzania wa Awamu ya Tano, hali inayowezesha matokeo na mapendekezo yake kusaidia kupanga vipaumbele na maboresho ya sekta ya afya nchini.

Ripoti hiyo inatambua maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Tanzania katika miaka ya karibuni. Mafanikio hayo ni pamoja na upanuzi wa huduma za saratani na ongezeko kubwa la wataalamu bingwa wa saratani, ambapo idadi ya wataalamu hao imeongezeka kutoka watano pekee mwaka 2006 hadi kufikia 65 mwaka 2025.

Waziri huyo pia alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kinga na ugunduzi wa mapema wa saratani, ikiwemo kupanuliwa kwa chanjo za HPV na Hepatitis B, kuimarishwa kwa huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, kuboreshwa kwa huduma za uchunguzi na upigaji picha, kupanuliwa kwa huduma za mionzi tiba, kuimarishwa kwa huduma za saratani kwa watoto pamoja na maendeleo ya huduma za tiba saidizi.

Licha ya mafanikio hayo, Mchengerwa alikiri kuwa Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa katika kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa saratani. 

Ripoti hiyo inakadiria kuwa nchini kulikuwa na takribani visa vipya 44,931 vya saratani na vifo 29,743 vilivyohusiana na saratani mwaka 2022.

Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa ni ucheleweshaji wa uchunguzi na wagonjwa kufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa, upatikanaji mdogo wa huduma maalumu maeneo ya vijijini, upungufu wa wataalamu wa afya, uhaba wa miundombinu ya uchunguzi na patholojia, muda mrefu wa kusubiri huduma za mionzi tiba, upungufu wa huduma za tiba saidizi pamoja na gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa.

“Mapitio haya yameainisha maeneo ya kipaumbele katika kuimarisha udhibiti wa saratani nchini Tanzania, ikiwemo kuandaliwa kwa Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Saratani wenye gharama na unaotegemea ushahidi, kuimarishwa kwa mifumo ya uongozi na uratibu pamoja na kuhakikisha upatikanaji sawa wa huduma bora za saratani nchini kote,” alisema Mchengerwa. 

Aliwahakikishia wajumbe na washirika wa maendeleo kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo kwa kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa.

“Tutaendelea kushirikiana kwa karibu na IAEA, WHO, IARC, washirika wa maendeleo, mashirika ya kiraia, taasisi za kitaaluma pamoja na wadau wote ili kuboresha matokeo ya huduma za saratani kwa wananchi wetu,” alisema.