Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Tanzania imezitaka taasisi za posta Afrika kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali kwenye shughuli zote ili kuendeleza biashara mtandao na kufukisha huduma zaidi za kifedha kwa jamii.

Akifungua mikutano ya kamati mbalimbali za Umoja wa Posta Afrika (PAPU) inayoendelea jijiji Arusha hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Selestine Kakele, amesema matumizi ya TEHAMA yataongeza,kasi, ubora na ufanisi wa huduma za posta, barani Afrika.

Mikakati ya kidijitali pia itachangia kujumuisha na kuboresha maisha ya watu wengi zaidi katika mfumo wa kifedha, aliozidi kuongeza nchini Tanzania na Barani Afrika.

Katibu Mkuu Mtendaji wa PAPU, Sifundo Chief Moyo; alimwambia Naibu Katibu Mkuu kwamba Umoja huo unatekeleza mikakati muhimu ili kufikia maono ya waanzilishi wake ya kuiunganisha Afrika kupitia posta.

Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono Umoja huo na kuwezesha kukamilika jengo la Makao makuu ya PAPU, jijini Arusha, Tanzania.

Jengo hilo, refu kuliko yote Kanda ya Kaskazini, limejengwa kwa ubia kati ya Umoja huo (PAPU) na Serikali ya Tanzania, kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Kamati za PAPU zinazokutana Arusha kati ya Agosti 24 na 28 zinahusika na Utawala na masuala ya kiufundi. Zitafuatiwa na mkutano wa Baraza la Utendaji la Umoja huo.

PAPU, yenye makao makuu yake Arusha, imepanga mikutano kadhaa itakayotangulia uzinduzirasmi wa jengo la umoja hupo tarehe 2 Septemba; utakaofanywa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. Mikutano hiyo ni pamoja na wa mawaziri wa sekta ya posta tarehe 1 Septemba, 2023.

Shirika la Posta Tanzania (TPC) ni miongoni mwa taasisi za posta Afrika zinazotekeleza mikakati ya kujipanga upya kutumia TEHAMA kutoa huduma.

Chini ya Mpango wa Tanzania ya Kidijitali, TPC imefungua vituo vya huduma za pamoja ambapo huduma mbalimbali za serikali na taasisi za umma zinapatikana. Hizo ni pamoja na usajili wa kampuni, maombi ya pasipoti na vibali
mbalimbali.