Mdhibiti wa viwanja vya ndege nchini Tanzania amekanusha kuruhusu utoroshwaji wa wanyamapori kutoka mbuga ya kaskazini hadi nchi za Mashariki ya Kati.

Inafuatia madai kwenye mitandao ya kijamii kuwa wanyama pori hao walikuwa wakisafirishwa kwa ndege za mizigo kutoka Loliondo, karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hadi Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilizitaja tuhuma hizo kuwa ni “uongo mtupu” na kubainisha kuwa uwanja wa ndege wa Loliondo si sehemu maalumu ya kuingia au kutoka.

Kulikuwa na madai kuwa ndege iliyokuwa imebeba wanyamapori ilionekana tarehe 26 Agosti, lakini TCAA ikapinga ikisema safari ya mwisho ya kwenda Loliondo ilikuwa Julai 19 na ina kiwanja maalumu chenye mizigo ya kawaida.

“Mamlaka ina mfumo wa ufuatiliaji wa wakati halisi na safari zote za ndege za kimataifa huingia na kutoka kupitia viwanja maalum vya kuingia/kutoka kama vile Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Abeid Karume (AAKIA),” ilisema katika taarifa.

Imesema taarifa hizo zinalenga kuchafua taswira ya nchi na kuwataka Watanzania kuzipuuza.

By Jamhuri