Tanzania yang’ara mkutano wa CITES nchini Panama

Tanzania imechaguliwa kuwa Mjumbe wa Akiba wa Kamati Kuu upande wa Kamati ya Wanyamapori na mjumbe wa Kamati ya Mimea kwa kipindi cha miaka mitatu (3) kwa nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyohatarini kutoweka CITES.

Hayo yamejili wakati wa mkutano wa 19 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyohatarini kutoweka CITES uliofanyika, nchini Panama kuanzia Novemba 14 hadi 25, 2022 na kufunguliwa na Makamu wa Rais wan chi hiyo Mhe. Jose Gabriel Carrizo.

Akizungumza mara baada ya kufikiwa kwa uamuzi huo, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana akiwa ameongoza ujumbe kutoka Tanzania amesema kuchaguliwa kwa Tanzania katika nafasi hizo za maamuzi kwa kipindi cha miaka mitatu kunaipa nafasi nzuri ya kusimamia na kutetea masuala ya kimkakati yenye maslahi mapana kwa uhifadhi na biashara ya kimataifa ya mazao ya wanyamapori, misitu na uvuvi.

Aidha, Waziri Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema mkutano huo umejadili ajenda zipatazo 89 yakiwemo mapendekezo 52 ya kuweka, kuondoa au kubadilisha hadhi ya wanyamapori na mimea katika makundi ya Mkataba wa CITES ambapo Tanzania imeshiriki kujadili mapendekezo 16 ya kuweka Wanyamapori na mimea katika makundi ya Mkataba wa CITES na agenda 24.

Jumla ya Nchi Wanachama 153 zimeshiriki katika Mkutano huo na zikiwakilishwa na washiriki takribani 3,000 waliojadili masuala ya kimkakati kuhusu biashara ya kimataifa ya wanyamapori na mimea iliyohatarini kutoweka, uwindaji wa kitalii, uhifadhi wa wanyamapori jamii ya tembo, simba, chui, faru, usimamizi na utunzaji wa shehena za meno ya tembo na mchango wa uhifadhi kwa maendeleo ya jamii.

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi chana huku Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini, Dkt. Maurus Msuha akiongoza timu ya watalaam iliyojumuisha wahifadhi wa wanyamapori, misitu na viumbe bahari wakiwa na jukumu la kuhakikisha maamuzi katika Mkutano huo yanafanyika kwa kuzingatia utafiti, taarifa za kisayansi, taarifa za biashara na uzoefu uliopatikana katika uhifadhi.