Mmiliki mpya wa Twitter Elon Musk amesema akaunti Twitter ya Donald Trump imerejeshwa baada ya kufanya kura ya maoni ambapo watumiaji waliunga mkono hatua hiyo.

“Watu wamezungumza,” aliandika Bw Musk, akisema kuwa 51.8% ya zaidi ya watumiaji milioni 15 wa Twitter walipiga kura ili marufuku hiyo iondolewe.

Lakini rais huyo wa zamani wa Marekani huenda asirudi jukwaani, akisema mapema: “Sioni sababu yake”.

Akaunti yake ilisitishwa mnamo 2021 kutokana na hatari ya kuchochea ghasia.

Uongozi wa awali wa Twitter ulichukua hatua siku chache baada ya wafuasi wa Donald Trump kuvamia Ikulu ya Marekani jijini Washington DC tarehe 6 Januari.

Mamia ya waandamanaji waliingia kwenye jumba hilo huku Bunge la Marekani likijaribu kuthibitisha ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa urais. Ghasia zilizofuata zilisababisha vifo vya raia wanne na afisa wa polisi.

Mara tu baada ya ghasia hizo, akaunti za Donald Trump za Facebook, Instagram na YouTube, ambazo zote zilikuwa na makumi ya mamilioni ya wafuasi – pia zilisimamishwa.