Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Meli ya watalii ya Norwegian, inayomilikiwa na kampuni ya Norwegian Cruiseline Holdings ya Marekani, kutoka nchini Norway yenye urefu wa mita 294 imewasili katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa na jumla ya Wageni 2000 ambapo wageni 1100 walishuka katika bandari ya Zanzibar na kuelekea katika vivutio mbalimbali vikiwemo Ngorongoro na Serengeti kupitia ndege za kukodi na hatimaye wataungana na abiria wenzao katika bandari ya Dar es Salaam na kuendelea na safari.

Hata hivyo, wageni zaidi ya 300 wameshuka katika bandari ya Dar es Salaam na kufanya matembezi katikati ya jiji la Dar es Salaam (City Tour) kupitia wakala wa utalii.

Akizungumza katika mapokezi hayo, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho amesema ujio wa meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 4,700 kutafungua milango kwa wadau wengine wenye meli kubwa zaidi duniani kutia nanga kwenye bandari hiyo.

Aidha, amesema maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika kupitia mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) yamechangia ujio wa meli hiyo na kwamba itasaidia kuchochea kuja kwa watalii wengi zaidi nchini.

Pamoja na mambo mengine ameongeza kuwa malengo ya bandari hiyo ni kuhudumia meli zenye urefu wa mita 305 hadi 350.