Bilioni moja zatumika miradi ya ujirani mwema

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mara

Wananchi wanaoishi jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) wamelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kufanikiwa kusimamia kiadilifu miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh 1,034,750,990.

Wakizungumza na JAMHURI Digital kwa nyakati tofauti, wakazi wa wilaya jirani na Senapa wamesema miradi yote imejengwa kwa kiwango cha juu.

“Ni kutokana na usimamizi wa maofisa wa Senapa. Hawa wamekuwa wakipita mara kwa mara kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa miradi.

Mhifadhi Mkuu wa Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Moronda Moronda

“Kwa kweli hili ni jambo la kufurahisha sana kwa kuwa linaonyesha namna sahihi ya kusimamia fedha za umma,” amesema Mwenyekiti wa Magesa Mtatiro, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kebisongo wilayani Bunda, kijiji ambako kimejengewa nyumba ya kisasa ya walimu.

Kauli yake inaungwa mkono na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bunyunyi, Sauda Said, akisifia madarasa matatu yaliyojengwa shuleni hapo.

Jumla ya Sh 927,122,340 zimetolewa na TANAPA na wadau wake kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia ujirani mwema, huku wananchi wakichangia asilimia 10 ya gharama, ambayo ni Sh 107,628,650; hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tanapa.

Miradi hiyo imetekelezwa katika vijiji vya wilaya za Tarime, Serengeti, Bunda, Busega, Bariadi, Itilima, Ngorongoro na Meatu kati ya mwaka 2018/19 na 2023/24.

Barabara, madaraja, madarasa, nyumba za walimu, zahanati, nyumba za waganga na ujasiriamali ikiwemo ufugaji nyuki kupitia Benki ya Hifadhi na Jamii (COCOBA), ni miongoni mwa miradi hiyo.

Mhifadhi Mkuu wa Senapa, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Moronda Moronda, amesema Rais Dk. Samia amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono uhifadhi, akimtaja kama ‘mhifadhi namba moja’.

Moja ya miradi inayotekelezwa na TANAPA

Kuhusu uhusiano wa TANAPA na taasisi za kimataifa kama Frankfurt Zoological Society (FZS) uliofanikisha kuifikia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW), moja ya wadhamini wa miradi, Moronda anasema ni kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

“Nyerere alisema kwamba Tanzania itashirikiana na mataifa mengine duniani katika jitihada za kuwahifadhi wanyama wa porini,” amesema Moranda.

Maneno haya ni kauli ya Baba wa Taifa kuhusu uhifadhi yamo katika kile kinachofahamika kama ‘The Arusha Manifesto’ (Ilani (Azimio) ya Arusha).

Maneno haya yamewekwa langoni mwa Ofisi ya Makao Makuu ya TANAPA jijini Arusha ili kila mhifadhi ayasome na kuyakumbuka.

Moronda anawashukuru majirani wa Senapa kwa ushirikiano wanaouonyesha na kuwezesha kupungua kwa matukio ya ujangili hifadhini.

Robert Masobeji