Na Mwamvua Mwinyi, jamhuriMedia, Pwani

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ametoa rai kwa mawakili wa Serikali , kila mmoja kutimiza wajibu wake na kufuata maadili na miiko kwenye majukumu yao.

Aidha amewaasa kuwa waadilifu na kutenda haki wakati wa kutimiza majukumu yao .

Akifungua mafunzo ya siku tatu ya Uongozi kwa Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yaliyoshirikisha Wakuu wa Idara ya vitengo na Mawakili wa Serikali wafawidhi wa mikoa 17 wilayani Kibaha, mkoani Pwani, Feleshi amewaeleza ,ili kuongeza ufanisi watakaguana na wasije kulaumiana .

Vilevile aliwataka ,kujituma na kuwa na maarifa mapya ili kufanya kazi zao kwa ufanisi.

“Mafunzo haya yatasaidia kuwajengea uwezo katika uandaaji wa kanuni na miongozo kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi, kujifunza mashauri ya haki za binadamu, uhitimishwaji wa tuzo za usuluhishi, namna taasisi nyingine zinavyosajili ,kusimamia mashauri kupitia mifumo ya TEHAMA hususan ofisi ya Taifa ya mashtaka na mahakama ya Tanzania” ameeleza Feleshi.

Pia Feleshi amewaasa, kuendelea kujifunza stadi za maisha kwa kuwa na maarifa mapya bila kukoma ,kwa kwenda sambamba na mabadiliko ya kidunia .

Pamoja na hayo Mwanasheria huyo Mkuu wa Serikali aliwasihi ,kutilia maanani elimu ya uwekezaji, namna ya kuongeza kipato ikiwemo ununuzi wa hisa, uwekezaji katika amana za Serikali, vipande vya UTT na hati fungani pamoja na uwekezaji katika ardhi.

Ameipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo ili kuongeza ufanisi kazini.

Awali Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende alisema, kwa miaka sita tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeleta mabadiliko makubwa.

Hata hivyo ameeleza ,kwa miaka mitatu sasa ,Ofisi hiyo imekuwa na desturi ya kufanya mafunzo na kikao cha faragha kwa ajili ya Menejiment ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na baadhi ya viongozi pindi wanapoingia mwaka mpya wa kalenda.

“Mafunzo haya yanalenga kuboresha ufanisi na kusaidia utatuzi wa ujumla wa changamoto mbalimbali ambazo zinazojitokeza katika utendaji kazi wetu.

Luhende aliweka wazi kuwa ,hadi septemba 2023 walifanikiwa kwa kuendesha mashauri 7,393 ambapo kati ya mashauri hayo 7,256 ni ya madai na 137 ni ya usuluhishi na kumaliza jumla ya mashauri 620 “:;mashauri 579 yalimalizika kwa njia za kimahakama na mashauri 42 yalimalizika kwa njia ya majadiliano ya nje ya mahakama.

“Mashauri yaliyomalizika kwa majadiliano tulimaliza mashauri yenye maslahi mapana kwa Serikali ikiwemo shauri la Ecodevelopment in Europe na wenzake dhidi ya Serikali na shauri la Winshear dhidi ya Serikali” amefafanua Luhende.

“Shauri baina ya CRMBEG-CRCEG JV for Mtwara Port Project dhidi ya Bandari Tanzania, shauri la DP World, shauri la Twiga Cement na shauri la nyongeza ya muda wa jaji Mkuu pamoja na mashauri mengine” ameongeza.

Pamoja na hayo Luhende alieleza, mwaka 2024 nchi inapotarajia kufanya chaguzi za Serikali za Mitaa na mwaka 2025 Uchaguzi Mkuu ,wanategemea kuboresha utendaji kazi wao.

Sambamba na hayo, mwaka wa fedha 2022/2023 ofisi hiyo imeweza kupata ongezeko la bajeti kutoka bilioni 12.8 hadi kufikia bilioni 17.075 ,ikiwa ni ongezeko sawa na asilimia 25.

By Jamhuri