Na WAF – Geneva, Uswisi

Wadau wa maendeleo wa Sekta ya Afya wameipongeza Tanzania kwa kuanzisha mpango jumuishi na shirikishi wa wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii utakaowafikishia wananchi huduma za Kinga, Tiba na Elimu ya Afya mahali walipo bila vikwazo.

Wadau hao wameipongeza Tanzania baada ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kuwasilisha umuhimu wa kuwatumia wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) ikiwa ni mkakati wa kuimarisha utoaji wa huduma za Afya ngazi ya msingi na kufikia lengo la Afya kwa wote.

Waziri Ummy amesema hayo Mei 28, 2024 kwenye Mkutano uliofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 77 wa Shirika la Afya Duniani (WHO), unaoendelea Jijini Geneva nchini Uswisi uliowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Mkutano huo uliowakutanisha wadau wa maendeleo, Taasisi za Kimataifa pamoja na mashirika yasiyo ya Kiserikali ya ndani na nje ya nchi umekuwa na mafanikio.

“Wadau hawa pia wameahidi kushirikiana na Tanzania wakati wa utekelezaji wa mpango utakaoleta mabadiliko na kuboresha Afya za wananchi ikiwemo kutoa rasilimali watu na fedha kwa kuendelea kuwatumia wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii.” Amesema Waziri Ummy.

Katika mkutano huo pia ulio ambatana na mdahalo wa wataalam wabobezi wa Afya ngazi ya msingi kutoka ndani na nje ya nchi, walieleza kwa kina na kwa ushahidi namna mpango huo utakavyoleta mabadiliko na kuboresha Afya za wananchi.

Mkutano huo ambao unahudhuriwa na washiriki zaidi ya 200 wakiwemo Mawaziri wa Afya kutoka nchi za Afrika na mabara mengine, umedhihirisha wazi matarajio na mategemeo ya wadau kuwa mpango huo utakuwa wa mfano kwenye kuboresha uratibu wa afua mbalimbali za Afya zinazotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Wadau waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na Umoja wa Afrika, Shirika la Afya Duniani, UNICEF, Global Fund, Botnar Fondation, Susan Buffet Thompson Foundation (STBF), PEPFAR, CDC, Swiss – TPH na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi.