Tuzo za Umoja wa Mataifa za Ubunifu katika Huduma za Umma ‘UN Public Service Innovation Awards’ zimetolewa leo Juni 26 mwaka huu, nchini Korea Kusini kwenye Kilele cha Wiki ya Huduma kwa Umma ya Umoja wa Mataifa ‘UN Public Service Week’.

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa 72 zimeshiriki ambapo mifumo 400 iliwasilishwa na mifumo 15 ilishindinda tuzo ukiwemo wa e-Mrejesho.

Kutoka Afrika nchi zilizoshiriki na kushinda tuzo hizo ni Tanzania na Afrika Kusini pekee.

Wiki ya Huduma kwa Umma ya Umoja wa Mataifa ni tukio la kila mwaka linaloadhimishwa kimataifa, kwa lengo la kusherehekea thamani na umuhimu wa huduma ya umma kwa jamii.

Tukio hili linasisitiza kutambua mchango wa watumishi wa umma na kuhamasisha vijana kuchagua kazi katika sekta ya umma.

Wiki hii kwa kawaida hujumuisha matukio, sherehe za tuzo, na majadiliano kuhusu jinsi ya kuboresha ufanisi wa utoaji huduma kwa umma duniani kote.

Mfumo wa e-Mrejesho unawawezesha wananchi kutuma kero au malalamiko, maoni, maswali, na pongezi kidijiti kwenda katika taasisi yoyote ya umma na kisha kupata mrejesho wa utekelezaji wake kidijiti mahali walipo.

Mfumo huu umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mfumo wa e-Mrejesho unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya 15200# na kisha kuchagua namba 9 na kisha namba 2, njia zingine ni kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni tumizi (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye Play Store na Apple Apps Store, na kwa njia ya Tovuti ya e-mrejesho.gov.go.tz.