šThe Hague, Uholanzi.
Tanzania imewaalika Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU) kuchangamkia fursa za uwekezaji nchini, hususani katika Sekta za Madini, Kilimo, na Sekta ya Dijitali, huku Serikali ikiahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji hapa nchini.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, wakati akifungua Jukwaa la Uwekezaji na Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania (EU -Tanzania Investment and Business Forum) jijini The Hague, nchini Uholanzi, akisisitiza kuwa wawekezaji wa Ulaya hawana sababu ya kusita kufanya maamuzi ya uwekezaji kutokana na utayari wa Serikali kushirikiana nao.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alisema kuwa Sekta ya Madini ni eneo muhimu la ushirikiano kati ya Tanzania na EU, akisisitiza kuwa wakati umefika wa kuhamisha majadiliano na fursa zilizopo kwenda kwenye utekelezaji wa uwekezaji halisi.
Mbibo aliwakaribisha wawekezaji wa Ulaya kushirikiana na Tanzania katika utafiti wa kijiolojia, tathmini ya rasilimali, maendeleo ya teknolojia na uzalishaji wa madini unaowajibika, akieleza kuwa taarifa sahihi za kijiolojia ni msingi wa maamuzi sahihi ya uwekezaji na uendelezaji endelevu wa migodi.
Katika jukwaa hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Eng. Ally Samaje alieleza fursa za madini muhimu nchini, ikieleza kuwa maeneo makubwa bado hayajafanyiwa utafiti wa kina, na kwamba fursa za ushirikiano zinahusisha utafiti wa kina (High Resolution Airborne Geophysical Survey), tafiti za jiolojia, jiokemia na jiofizikia, pamoja na kuimarisha uwezo wa maabara na mifumo ya taarifa za kijiosayansi.
Aidha, akizungumza katika jukwaa hilo, Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Theresia Numbi alieeleza kuwa Kampuni za Ulaya zinaweza kuwekeza kupitia ubia na Kampuni za Kitanzania, kuanzisha uzalishaji, uunganishaji wa mitambo, matengenezo, uhandisi na huduma za kitaalamu, pamoja na kuleta teknolojia, mitaji na utaalamu katika madini muhimu, uchakataji, uboreshaji wa kidijitali, usimamizi wa mazingira na nishati jadidifu.
Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Caroline Chipeta, alisema jukwaa hilo ni muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kisiasa kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, huku akisisitiza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, hususani katika madini muhimu na ya kimkakati.







