Katika makala yangu wiki iliyopita, nilieleza kuhusu chanzo cha nchi yetu kuwa maskini, wakati Mwenyezi Mungu ametujaalia rasimali nyingi kuliko mataifa mengine duniani kote, kwamba ni laana ambayo imetokana na viongozi wetu waliotangulia kuilaani Israel.

Wako baadhi ya wasomaji waliokubaliana nami kwa kunipigia simu moja kwa moja na wengine waliotuma ujumbe mfupi wa maneno (sms) wakiungana nami kwa yote niliyoyaeleza.

Nilieleza kwamba kazi anayoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, ya kukomesha uhuni wa kila namna unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji serikalini ya ‘kutumbua majipu’, inaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana iwapo hatatoa kauli za laana dhidi ya taifa la Israel.

Miongoni mwa walioniunga mkono baada ya kuisoma makala hiyo ni msomaji wetu mwenye namba 0768 375375 aliyesema “nchi kama hii bila kuwa na Rais kama huyu, sijui tulikuwa tunaelekea wapi?” 

Lakini msomaji mmoja wa makala hiyo yeye alijielekeza zaidi kwenye ushabiki wa kidini licha ya kukubaliana nami kwamba umaskini wa nchi yetu ambayo marais wa awamu ya tatu na nne hawakuwa na majibu kwa nini Tanzania yenye utajiri wa rasilimali iwe nchi maskini duniani?

Msomaji huyu ameshindwa kuelewa laana iko kwa kiwango gani nchini? Lakini nieleze kwamba ukiona nchi ina madini ya kila namna huku wananchi wakiendelea kuwa na umaskini na wengine wanaoishi maeneo ya migodi kuuawa kwa maelekezo ya wageni, hii ni laana.

Nchi iliyolaaniwa ina hifadhi nyingi za wanyama lakini wananchi wanaendelea kuwa maskini huku wakishuhudia mchana kweupe wanyama hai wakipakiwa kwenye ndege na kutoroshwa. Wageni wamelifanya shamba lao kwa umbumbu wa viongozi maslahi, hii ni laana.Tuna ardhi lakini wanaoitwa wawekezaji wameitwaa kama watakavyo na kuwaacha wananchi bila maeneo ya kilimo wala kufuga na kuwaacha wananchi wakiuana na mambo mengine mengi, hii ni laana.

Kwa kifupi, huyu anayepinga huku akielekeza hoja kwenye ushabiki wa kidini, anapaswa kuelewa kwamba nchi yetu imekaa katika laana kwa muda mrefu kwa kuilaani Israel.

Rais, Dk.Magufuli amesema anapochukua hatua yeye si kichaa, si dikteta, si shetani wala si mnyama, ila ni mpole, lakini amefika mahali lazima afanye hivyo kwani ndani ya Serikali yanafanyika mambo ya ajabu. Kiu ya Watanzania wengi ilikuwa ni kumpata Rais mkali na mzalendo wa kweli, atakayepambana na rushwa na ufisadi ambao umeigharimu nchi kwa tawala zilizopita. Nchi yetu ilionekana ni shamba la bibi lililokosa mlinzi wala mtunzaji.

Lakini baada ya Dk Magufuli kuingia madarakani, kundi la ‘watafuna nchi’ lililojiwekea mirija kuwanyonya Watanzania kama watakavyo kwa kujijenga kikamilifu ndani ya CCM na Serikali yake, limeanza kutapatapa na kudai Rais ni dikteta, mbabe, hataki kusikia ushauri wa wenzake wala hana huruma na watu.

Biblia Takatifu (MWANZO 12: 1-3, BWANA akamwambia Abrahamu, ‘Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa …nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe  jamaa zote za dunia watabarikiwa’).

Katika uzao huo huo wa Abrahamu, tunaona Yakobo akibarikiwa na kuitwa Israeli (MWANZO 32: 24-29) (MWANZO 27:29). Laana ndiyo chanzo kikuu cha madudu yote yanayofanyika serikalini sasa. Nchi ina kila kitu, lakini inaitwa maskini duniani.

1429 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!