Mwanadamu ni kiumbe tofauti na viumbe wanyama wengineo hapa duniani.

Kimaumbile viumbe wanyama wote wako sawa kwa maana wanatawaliwa na silika au vionjo vya miili.

Mathalani, kila mnyama anaupenda uhai, hivyo anatambua adui wake na silika inamwelekeza namna ya kujikinga (protective instinct), anasikia maumivu (feeling), anaona (sight), ananusa (smell), hasa wanyama wanaowinda na kula wanyama wengine. Hizi silika ndizo zinazomkinga na kumwezesha aishi kwa usalama pale anapoishi. 

Basi mwanadamu pamoja na kupewa na Mwenyezi Mungu hizo silika, ameongezewa kitu kinachoitwa utashi. Sasa zawadi hii kubwa ya itashi ndiyo pekee inayomtofautisha huyu kiumbe mwanadamu na hao viumbe wanyama wengine.

Utashi ni uwezo pekee aliojaaliwa mwanadamu na kwa uwezo huo ana ile hali ya kuweza kuchagua nini afanye na nini asifanye. Kwa hiyo basi kila mwanadamu anapotenda jambo amekuwa ameamua na kuchagua kutenda hivyo na ni kwa hiari yake binafsi.

Kwa maana hiyo matendo yote haya atendayo mwanadamu, ni matokeo ya ule utashi alionao wa kuamua mambo. 

Sasa basi kuna hali zinatokea duniani kitaalamu tunaita ‘mazingira’. Itokeapo hali hiyo hapa mwanadamu analazimishwa kujirekebisha ili aweze kuishi katika mazingira husika. Kibiolojia hali hiyo ya kiumbe kujirekebisha kulingana na mazingira inaitwa ‘adaptation to environment’. Ikijatokea hali namna hiyo ndipo mwili wa mnyama binadamu nao unajirekebisha ili uweze kuendana na hali hiyo ya mazingira alipo. 

Mfano hai ni wa kinyonga, mnyama anayejirekebisha rangi ya mwili kulingana na mahali alipo. Hujibadilibadili rangi zake tunaita kwa Kiswahili sanifu kujikamafleji (camouflage). 

Hali ya mbadiliko wa mazingira inaeleweka vizuri sana kule nchi za ukanda wa dunia wenye baridi sana na joto kidogo (cold and temperate zones). 

Nchi zote za Ulaya wanaelewa hali ya mazingira ndiyo maana wamegawana nyakati za mazingira yao. Hali ya kubadilika huko kwa mazingira kumegawanyika katika sehemu tofauti. Wakati wa baridi kali na theluji wameita ‘winter’.

Kunaingia kipindi mimea inaanza kuchipua sasa wanaita ‘spring’ sisi tunaita kipupwe na wakati kuna jua kali na kwa saa nyingi wenzetu ndipo wanaita ‘summer’ yaani kiangazi. Huko maisha ya watu huwa yanarekebishika kwa aina ya chakula na mavazi kwa kila kipindi cha hali ya hewa inavyobadilika.

Kuna sehemu duniani tunaita majangwani kama Sahara, Arabia, Kalahari na kadhalika. Kule wanadamu wanajua sana kujihifadhi kimavazi, ujenzi wa makazi na hata aina ya vyakula. 

Nimeelezea haya yote kukuonesha msomaji namna mwanadamu anavyotumia utashi wake kuamua anakuwaje katika mazingira fulani fulani.

Kamwe, mwanadamu huyu hayakimbii mazingira anamoishi bali yeye anayapokea, anakabiliana nayo na anajirekebisha (face the challenge and adapt to the particular situation or environment). 

Tatizo lililopo sasa kule Visiwani ni upatikanaji wa Serikali halali ya Mapinduzi. Hili ni tatizo la kihistoria na ni tatizo la kisiasa. Kwa upande wa historia, sote tunajua Visiwa vya Unguja na Pemba vimekuwa chini ya utawala wa Sultani wa Oman, Uarabuni, tangu enzi za kale ilipojulikana kama “The Sultan of Oman and Zanzibar” mwaka 1804.

Rekodi zinaonesha watawala wa Visiwani huko ni kuanzia yule Sultani aliyekiitwa Said Majid (1856-1870). Kutoka hapa ukoo huo wa Majid umetoa masultani kadhaa waliotawala Zanzibar. Mmoja anayejulikana sana ni huyu Said Baraghash (1870-1888). Kumbe huyu ndiye aliyefanya makubaliano ya utawala wa Visiwani kulindwa na Uingereza baada ya ule Mkutano Mkuu wa Berlin wa mwaka 1884 (after the Berlin Conference)

Matokeo ya Mkutano ule Bara la Afrika lilimegwa mapande mapande wakakabidhiana Wazungu wa Ulaya tukawa makoloni. Hivyo Zanzibar ikaangukia chini ya ulinzi wa Mwingereza (became British Protectorate). Basi inatosha hapa niseme tu kuwa utawala wa Waarabu ulififishwa nguvu zake na huo mfumo wa ulinzi (protectorate) wa Uingereza.

Wanaukoo wa Oman wakawa wanatawala mpaka usiku ule wa Januari 12, 1964 yalipotokea yale Mapinduzi Matukufu yaliyowakomboa Waafrika weusi kutoka makucha ya Waarabu.

Hapo mtawala wa Kiarabu aliyeitwa Sultani Jamshid bin Abdulla, alipinduliwa na akaikimbia Zanzibar na mpaka leo hii yuko nje ya Visiwa hivi. Huyu Sultani kwa kweli hakutawala sana. Babaake, Sultan Abdulla bin Khalifa, alitawala tangu 1910 mpaka hapo alipofariki Julai mosi, 1963 ndipo Sultan kijana akarithi. Lakini akapinduliwa baada ya miezi saba tu. (Tazama Historical Dictionary of Tanzania by Laura S Kurtz – Utangulizi uk. XII na uk. 80). 

Kwa mtazamo wa kisiasa mambo ni tofauti sana. Mpaka siku kabla ya Mapinduzi (Januari 12, 1964), Visiwa vya Unguja na Pemba vilipata sifa moja ya kuitwa Visiwa vya Amani. Licha ya mabadiliko kadhaa ulimwenguni katika maisha ya binadamu, Visiwa vya Zanzibar havikuathirika, bali vikawa kitovu cha amani, furaha na umoja bila kuwa hata na misuguano ya dini au ya ukabila.

Uvunjikaji wa amani, wala vurugu au fujo za aina yoyote havikupata kusikika kabla ya Mapinduzi. Inasemekana enzi hizo huko Visiwani kila ukutanapo na Mzanzibari mwenzako amkio lilikuwa moja tu ‘Asalam Aleikum’ hapo wote walijiona na kujisikia ndugu moja tu – ‘Wazanzibari’.

Lakini bwana, baada tu ya Mapinduzi yale ya Januari 12, 1964 hali ikageuka. Mambo yakabadilika huko Visiwani na nchi ikazongwa na jinamizi la uhasama. Kuanzia hapo Wazanzibari waligawanyika. Kukawa na makundi mawili. 

Kundi la Warabu mojawapo liliikubali ile hali, likaipokea wakabaki Wazanzibari ndiyo wanaoishi bila kinyongo hadi leo hii.

Lakini kulitokea kundi la mabwenyenye Waarabu walioghadhabika kupinduliwa utawala wa Sultani wao, wakakimbilia nje ya nchi wakiwa na fukuto na vinyongo vya kunyang’anywa tonge la wali kinywani. Kwa kiburi kikubwa na kwa ghadhabu hawakutaka kabisa kutawaliwa na weusi (waliokiwaita magozi). Hili kundi si dogo na lina nguvu kifedha na ushawishi (influence) mkubwa huko nje. Limebaki kumezea mate nchi nzuri ya Zanzibar wakati linaishi nje ya bara la Afrika. 

Kipo kijarida kimoja kimeandika hivi na nukuu “during recent years, there have been dramatic social and economic upheavals in the Stone Town. Following 1964 Revolution, many of the WEALTHIEST merchants and craftsmen, ARABS as well as INDIANS left Zanzibar abandoning their fine old houses and Bazaar shops. The Revolutionary Government subsequently CONFISCATED many of the abandoned buildings, converting them into mult-family housing units and allocated them to LOW-INCOME RESIDENTS”. (Tazama Zanzibar: Home of cloves, kind people uk. 11). 

Sidhani kwamba kuna haja ya kutafsiri hayo. Lakini kuanzia hapo penye mgawanyiko wa Wazanzibari baada ya Mapinduzi, misuguano isiyokoma imekuwa jambo la kila siku. Ni mawimbi yanayoisumbua Serikali yoyote ya Zanzibar mpaka leo hii.  

Wazanzibari kadhaa wametoa mawazo yao katika magazeti juu ya huo msuguano wa kisiasa huko Visiwani. Hata huko kukwama kwa mazungumzo baina ya viongozi wa CUF na wa CCM wametoa sababu za viongozi wao kutokufikia makubaliano kwa faida ya Wazanzibari wote hasa tunaowaita wazalendo. 

Nitoe mifano michache ya mawazo ya Wazanzibari hawa. Balozi Amina anasema hivi, “pale Zanzibar kuna siasa za ndani na siasa za nje ya nchi. Zile siasa zinazoanzia nje ya nchi ndizo zinazoivuruga Zanzibar, kwa maana hiyo suala hapo siyo kurudia uchaguzi tu, ni kuangalia mambo yote hayo na kuona namna gani yanaweza kudhibitiwa” (Balozi Amina katika Mwananchi toleo No. 5664 la Januari 30, 2016 uk. 2).

 

Itaendelea

1336 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!