Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Balozi wa Namibia Nchini Tanzania Lebbius Tangeni Tobias,amefanya ziara rasmi ya kikazi katika Chemba ya Biashra, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Chemba hiyo, Paul Koyi katika ofisi za Makao Makuu ya TCCIA, Zilizopo jijini Dar es Salaam.

Tobias alifanya ziara hiyo katika ofisi hizo za TCCIA ikiwa ni mojawapo ya mbegu za awali inayokwenda kuzaa matunda ikiwemo kuimarisha na kukuza uhusiano wa kibiashara baina ya Mataifa mawili ya Tanzania na Namibia Julai 29,2022.

Katika majadiliano hayo,Tobias alimueleza Rais wa TCCIA Mheshimiwa Koyi kuwa, hali ya biashara baina ya Tanzania na Namibia imekuwa si ya kuridhisha kwa siku hizi za usoni na hivyo kuhimiza kuwekwa kwa mikakati ya pamoja itakayokwenda kuhuisha uhusiano huo na kuuimarisha zaidi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Katika kutafuta mwarobaini wa changamoto hiyo ya biashara kuzorota baina ya mataifa hayo mawili, viongozi hao wamekubaliana kuweka mpango wa kusini hati ya makubaliano (Memorandum of Understanding) baina ya chemba ya Biashara ya Namibia na chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo ya Tanzania kati ya tarehe 6 mpaka 8 ya Septemba mwaka huu 2022, kama mpango mkakati utakaowezesha kufikia lengo la kuimarisha hali ya biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili ya Namibia na Tanzania.

Aidha balozi Tobias ameeleza kuwa kampuni nyingi za kutoka Namibia zingenda kufanya Biashara na Tanzania hususani kwa bidhaa kama za vyakula kama mchele, matunda na mbogamboga.

Balozi Tobias ameambatana pamoja na maofisa wawili kutoka ubalozi wa Namibia nchini Tanzania, akiwemo Saara Amukugo ambaye ni Mshauri Ubalozini hapo Huku kwa upande wa TCCIA, Koyi aliungana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA Nebart mwapwele pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Biashara cha TCCIA Ndugu mercy Philipo walioambatana na Rais Koyi katika Kikao hicho cha majadiliano hayo rasmi, yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa Kibiashara baina ya Tanzania na Namibia

By Jamhuri